Na. Tamimu Adam, Jeshi la Polisi.

WATANZANIA wametakiwa kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu JK. Nyerere kwa kuchukia vitendo vya uhalifu na wahalifu vinavyotokea katika jamii ili kuhakikisha taifa la Tanzania linaendelea kuwa la amani, Usalama na utulivu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.

Hayo yalibainishwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso wakati akijibu swali lililomtaka yeye kama mwanausalama anataka watanzania wamuenzi vipi muasisi wa taifa la Tanzania kwani alikuwa ni kiongozi wa amani kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Akimzungumzia Baba wa Taifa, Senso alisema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mwenye msimamo imara, alikuwa anachukia vitendo vyote vya ubadhilifu, unyanyasaji, uchochezi wa kidini, kisiasa ikiwa ni pamoja na vitendo vya uhalifu, vitu ambavyo ni hatari kwa taifa linalohitaji ushirikiano wa pamoja baina ya Serikali na wananchi wake ili liweze kujikwamua kimaendeleo hususani kiuchumi, kisisasa yakiwemo maendeleo ya kiulinzi na usalama.

Alibainisha kuwa, miongoni mwa mbinu za kupata maendeleo ya kiusalama ni ushirikiano wa jamii katika kubaini na kufichua uhalifu na wahalifu katika makazi yao kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au kushirikiana na askari tarafa waliokwisha sambazwa katika tarafa kote nchini ili kushirikiana na familia katika kutatua kero za kiusalama zinazowakabili.

“familia zikiwa salama, tutakuwa na mtaa salama, Mitaa ikiwa salama, tutakuwa na kata salama, Kata zikiwa salama tutakuwa na tarafa salama, Tarafa zikiwa salama tutakuwa na Wilaya salama, Wilaya zikiwa salama, tutakuwa na Mikoa salama, Mikoa ikiwa salama, Tutakuwa na Taifa salama” alisema Senso.

Pia alitoa wito kwa wananchi kutowaonea haya wahalifu badala yake waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa kuwa kosa la jinai huwa halifutiki, taarifa hizo ni muhimu kwani zitasaidia kukamatwa kwa wahalifu waliotenda uhalifu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Aliongeza kuwa mhalifu ni adui namba moja wa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla kwani unyang’anya au kuiba mali za mtu au umma ambazo zimepatikana kwa taabu, jambo ambalo hata baba wa taifa alikuwa akilikemea kwani linarudisha nyuma maendeleo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...