Na Freddy Macha

Alhamisi  jioni, Wazalendo na marafiki zao walishiriki misa maalum ya kuiombea Tanzania  ndani ya kanisa mashuhuri  la Westminster Abbey kuadhimisha miaka 50 ya muuungano.

Misa hizi hutayarishwa kila mwaka kwa heshima ya nchi za Jumuiya ya Madola. 
Mgeni rasmi alikuwa Balozi wetu Uingereza Mheshimiwa Peter Kallaghe, maofisa  ubalozini na wawakilishi wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (British-Tanzania Society)....

Kwaya ya Chuo cha Lancing, iliimba nyimbo za kizamani za Kizungu na Kikristo katika mahadhi yaliyorembwa na vinanda na maandiko matakatifu.  Westminster Abbey iliyo eneo la majengo mahsusi ya kiserikali na saa maarufu - Big Ben,  iliasisiwa  mwaka 1245 na Mfalme Henry wa Tatu. Ni moja ya majumba yanayothaminiwa na kuheshimiwa  sana Uingereza. Toka mwaka 1066 watawala wa kifalme, watu mashuhuri na muhimu nchini huzikwa ndani humo. 

Kati yao ni  William Shakespeare na Charles Dickens (waandishi mashuhuri) ;mmisionari aliyesafiri Afrika Mashariki na Kati karne 19, Dk. David Livingstone; wanasayansi Isaac Newton na Charles Darwin. Vile vile Waziri Mkuu Wiston Churchill aliyeongoza taifa hili wakati wa vita vikuu vya pili vya Wazungu (1939-45).
 Mwili wa Baba wa taifa Mwalimu Nyerere uliwekwa hapa kutazamwa na kadamnasi kabla ya kusafirishwa Tanzania, Oktoba 1999.

Sala maalum kwa ajili ya marehemu Nelson Mandela ilifanywa Westminster mwezi Machi mwaka huu.
 Mbali na misa na mazishi -Westminster Abbey  huwa ukumbi wa  sherehe maalum. Mathalan miaka ya karibuni ndoa za mtoto wa Malkia Elisabeth (Prince Charles na Diana, 1981) na mjukuu William (2011) na Catherine,  zilisheherekewa hapa. 

Akizungumza kwa Kiswahili na Kiingereza baada ya sala, Balozi Kallaghe aliwashukuru wote waliohudhuria.
“Ni heshima iliyoonyeshwa na watu wa madhehebu mbalimbali kujumuika pamoja kuombea taifa letu na kumtakia kila Mtanzania mazuri,” alisema.

Kati ya Watanzania niliozungumza nao  ni Zarina na Zehra Jafferji wa dhehebu la Kibohra waliolitakia taifa letu  mema na mfanyabiashara Abubakari Faraji na Mariam Kilumanga wa jumuiya ya wanawake London (TAWA). 

“Watanzania ni ndugu moja,” alisema Mariam Kilumanga. “Ndani ya familia yangu tunao watu wa  dini kadhaa bila ubaguzi.”  

Mtanzania mshindi wa taji la Jumuiya ya Madola la Africa (Miss Commonwealth Africa 2013) Malkia Kassu, alisema ni kitendo cha amani kuwa Westminster Abbey na ishara ya matumaini kwetu sote.
Peter Kallaghe, akitoka kanisa maarufu la Westminster Abbey, alipohudhuria misa ya kuiombea Tanzania katika maadhimisho ya miaka ya muungano 50 Alhamisi jioni. Kati kati ni Trevor Francis wa jumuiya ya Uingereza na Tanzania (British Tanzania Society).
Balozi Peter Kallaghe akisalimiana na Watanzania wa madhehebu ya Kibhora waliohudhuria misa iliyotayarishwa kila mwaka kwa mataifa yaliyo ya Jumuiya ya Madola, jengo la Westminster Abbey, London.
Picha ya pamoja kwa baadhi ya washiriki wakiwa Balozi Mhe Peter Kallaghe.
Baadhi ya Watanzania waliohudhuria misa kanisa la Westminster Abbey.

Westminster Abbey kwa nje .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...