Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda
atakuwa mgeni rasmi katika hafla iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na
Madini ya kukabidhi hundi za ruzuku ya Dola za Marekani 500,000 kwa
wachimbaji wadogo 11 waliokidhi vigezo.
Hafla ya Utoaji wa hundi hizo kwa wachimbaji wadogo itafanyika mjini
Dodoma tarehe 9/4/2014 katika Chuo cha Madini ambapo Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiambatana na Naibu
Waziri anayeshughulikia Madini, Stephen Masele pamoja na watendaji
kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) pamoja na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania
(FEMATA) watashuhudia utoaji wa hundi hizo.
Ruzuku hiyo ya Dola za Marekani 500,000 imetolewa na Benki ya Dunia
kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio
chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
Kutolewa kwa hundi hizo ni matokeo ya mkataba ambao Wizara ya Nishati
na Madini iliingia na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili Benki hiyo iwe
Wakala wa kutoa mikopo na ruzuku kwa wachimbaji wadogo kwa niaba ya
serikali.
Mkataba wa uendelezaji wachimbaji wadogo ulioingiwa kati ya TIB na
Serikali unasisitiza ruzuku kutolewa kwa wachimbaji wadogo wenye
sifa ili kuwawezesha kufanya shughuli zao za uzalishaji mali, wakiwepo
wanawake wanaojishughulisha na utoaji huduma katika maeneo ya
uchimbaji mdogo.
Wachimbaji wadogo 11 watakabidhiwa hundi hizo za ruzuku baada ya
kukidhi vigezo vya kuwa na uzoefu wa uchimbaji mdogo usiupungua miaka
Tano, kuwa na leseni hai ya uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini
pamoja na kuwa na ushahidi wa upatikanaji wa mashapo au mali ghafi
inayohitajika kwa ajili ya mradi unaoombewa ruzuku.
Imetolewa na;
BADRA MASOUD
MSEMAJI WA WIZARA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...