Na Editha Karlo wa Globu ya Jamii,Kigoma
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Gombe school of Environment and Society (GOSESO) na mmiliki wa Gombe high school, Dkt Yared Fubusa ambaye pia ni kada wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ametangaza nia ya kugomba ubunge jimbo la Kigoma kaskazini kupitia chama hicho.
Akiongea na mtandao huu, Dkt Fubusa alisema kuwa ameamua kutangaza nia ya kugombea ubunge na kipaumbele cha awali ni kuboresha Elimu,huduma za afya,miundombinu.
Alisema vipaumbe vyake baada ya kuchaguliwa pia ni pamoja na zahanati ya Bitale kuwa na hadhi ya hospitali ya wilaya,ujenzi wa sekondari katika kata 14 , ujenzi wa soko katika mji mdogo wa Mwandiga ikiwa ni sambamba na ujenzi wa viwanda vya uchakataji wa juisi ya matunda matunda,kahawa na mchikichi ili kuongeza thamani ya bidhaa na kupunguza kero ya ajira kwa wananchi wa jimbo hilo.
Alisema endapo wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini watampa ridhaa ya kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atajitahidi kutengeneza fursa za ajira hasa za makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana na akina mama kwa kuishawishi Serikali itakayokuwepo madarakani,kuhakikisha inaleta wawekezaji mbali mbali jimboni.
Alisema ahadi hizo si za kubahatisha kwa kuwa anawafadhili na marafiki zake kutoka marekani ambao wapo tayari kumuunga mkono ili kuleta maendeleo katika jimbo la Kigoma Kaskazini,pia alisema wakazi wa vijiji vilivoporwa ardhi na hifadhi ya Gombe mwaka 1968 watafidiwa haki zao ambazo waliondolewa bila kufidiwa.
Aliongeza kwa kusema pia katika jimbo hilo kuna changamoto ya kuongezeka kwa chanzo cha mapato katika mwalo wa kijiji cha Kalalangabo kwa kujengwa forodha ili kuongeza mapato kwa halmashauri akiwa Mbunge atashughulikia hilo swala pia.
''Rais Jakaya Mrisho Kikwete ni kiongozi anayeunga mkono uthubutu wangu kwani mimi ni kijana pekee mzalendo ,jasiri na mwenye uchungu wa kuwaondoa watu wa jimbo la Kigoma kaskazini katika janga la umaskini kwa kuwa ametoa ajira zaidi ya watu 50 katika shule ya sekondari Gombe na timu ya Mvuvumwa”alisema Mgombea huyo mwenye Phd ya uchumi,maliasili na mazingira.
Dk.Fubusa alisema kwamba wananchi wanapaswa kutathimini uwajibikaji wa mgombea katika jimbo husika kwa kigezo cha mahusiano bora yenye maslahi kwa jamii hiyo ,ili kuepuka viongozi wanaokimbilia kuishi mijini baada ya kupata ubunge na kuwataka wananchi wasikubali kuchagua viongozi wa aina hiyo ambao wapo kwa maslahi binafsi.
Dk Fubusa ni mzaliwa katika kijiji cha Kiganza Kata ya Mwandiga Mkoani Kigoma ni msomi mwenye Phd ya Uchumi hivyo lengo lake la kutaka ubunge katika Jimbo la Kigoma Kskazini ni kushirikiana na wanakigoma kaskazini katika kuleta maendeleo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...