Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira
Na Eleuteri Mangi MAELEZO
29/09/2015
Serikali ya Tanzania na Poland zimeingia makubaliano ya ushirikiano yatakayosaidia kukuza sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo kupitia  Kampuni ya kutengeneza Matrekta ya Ursus kutoka nchini Poland itakayoanza kufanya kazi zake nchini Tanzania mwanzoni mwa mwaka 2016.

Akizungumza mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa makubaliano hayo kati ya Serikali ya Tanzania na  ujumbe wa wataalam wa kilimo kutoka nchini Poland ulioongozwa na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vjijini wa Poland Bi. Zofia Szalczyk jana jijini Dar es salaam, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kuinua sekta ya kilimo na kurahisisha upatikanaji wa matrekta hapa nchini.

Alisema Kampuni ya kutengeneza Matrekta ya Ursus kutoka  Poland imepewa jukumu la kuleta vipuri vya matrekta na kuviunganisha hapa hapa nchini ikishirikiana na Shirika la Uchumi na Maendeleo la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).

“Tumeingia mkataba na Seikali ya Poland ili kuinua na kuimarisha sekta ya kilimo nchini kupitia  uundwaji wa matrekta haya hapa nchini, kazi hii itasaidia kupunguza  kilimo cha jembe la mkono ambacho kinafikia asilimia 62  na  asilimia 38 iliyobaki inajumuisha kilimo cha jembe la kukokotwa na wanyamakazi “plau” pamoja na matrekta” Alisema.

Aliongeza kuwa Serikali itawajengea uwezo SUMA JKT ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo na  kuondoa hali iliyopo ya uagizaji wa matrekta yaliyounganishwa  ambayo hutumia gharama kubwa na kusababisha  wakulima wengi hushindwa kumudu gharama ya kuyanunua.

“Wakulima wataunganishwa na Benki ya kilimo nchini kwa kupewa mikopo mbalimbali ya kununua vifaa vya kutendea kazi mbegu pamoja na mbolea ili kukifanya kilimo kiwe cha kisasa zaidi” alisema Wasira.

Wasira alisema kuwa Maghala yaliyopo nchini yanauwezo wa kuhifadhi chakula tani 240,000 baada ya kukamilika ujenzi wa maghala hayo kutakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 446,000 za chakula ambapo zitatumika Dola za Kimarekani milioni 110 katika ujenzi wa maghala hayo.

Aidha, Wasira aliongeza kuwa ili kuwa na mafanikio katika sekta ya kilimo nchini, Serikali itapeleka wataalamu wa matrekta kila mkoa.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vjijini wa Poland Bi Zofia Szalczyk alisema kuwa hatua iliyofikiwa na Serikali ya Tanzania ni ya muhimu katika katika kuongeza tija katika uzalishaji kupitia sekta ya kilimo.

Alisema Poland imefanikiwa katika sekta ya kilimo kwa sababu inashirikiana na taasisi za kifedha za kimataifa ambapo ameisifu Tanzania kuchukua uamuzi huo ambao utaiwezesha kuwa na kilimo chenye tija.


Adha, ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na Waziri wa Fedha nchini na kuahidi kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...