Wakazi wa Kijiji cha Kindi Tarafa ya Kibosho Wilayani Moshi Mkoani  Kilimanjaro, wakiwa kwenye mazishi ya marehemu Eugeni Mboro mfanyabiashara  wa mahindi aliyeuawa kwa kukatwa na shoka nyuma ya shingo yake na kuporwa sh.700,000. 
Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Anthony wa Padua, Kijiji cha Kindi Tarafa ya Kibosho Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, Padri John Senya, akiongoza ibada ya mazishi ya marehemu Eugeni Mboro mfanyabiashara wa mahindi aliyeuwa kwa kukatwa na shoka nyuma ya shingo yake na kuporwa sh700,000.

Na Woinde Shizza, Moshi.
WANANCHI wa Kijiji cha Kindi Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro wamesema ili kukomesha mauaji ikiwemo tukio la kukatwa na shoka nyuma ya shingo kwa Eugeni Mboro kwa sababu ya sh. 700,000 wauaji hao wachukuliwe hatua. 

Mkazi wa kijiji hicho Richard Massawe alisema jana chanzo cha kifo hicho ni sh700,000 alizokuwa nazo Mboro baada ya kuuza mahindi yake ndipo baadhi ya watu aliokuwa nao kupanga njama za kumuua na kuzichukua fedha hizo. 

“Tunaomba serikali ichukue hatua kwani Mboro alikuwa ni mjasiriamali mdogo anayeibukia hapa Kindi na asiyekuwa na tatizo na mtu ila hao kina Gasto na Kisimati walishikwa na tamaa ya kumuua ili wachukue pesa,” alisema Massawe. 

Mjomba wa marehemu Joseph Mwacha aliiomba serikali kuchukua hatua kwa wahusika wote wa mauaji hayo kwani ndugu yao hakudhulumu kitu cha mtu ila ni roho mbaya zilizosababisha kifo hicho na kumpora sh700,000 zake. 

Hata hivyo, akiongoza ibada ya mazishi hayo, Paroko wa kanisa katoliki parokia ya Anthony wa Padua, Padri John Senya, aliwataka wakazi wa eneo hilo kupiga vita matukio ya uuaji kwa mtu asiye na hatia. 

“Tunapaswa kubadiliwa jamani watu Kindi kwani itafikia siku mtu ukisema umetoka Kindi watu watakuangalia mara mbili mbili hivyo unasema umetoka Kibosho badala ya kutaja eneo hili tulipozaliwa,” alisema Padri Senya. 

Kwa upande wake, kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Ramadhan Mungi alisema mwili wa Mboro ulikutwa kwenye shamba la Michael Makabili huku akiwa na jeraha nyuma ya shingo lililotokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali. 

Kamanda Mungi alisema pia marehemu aliibiwa fedha zake sh700,000 na wanawashikilia watuhumiwa wawili kwa uchunguzi akiwemo Gasto Costa  (25) mkazi wa kijiji cha Kindi na mtu mwingine ambaye hakumtaja jina lake. 

“Huyu mtuhumiwa Gasto tulifanya upekuzi kwenye nyumba yake na kukuta kuna shuka lenye damu na nguo za marehemu Mboro ila huyu mtuhumiwa mwingine bado tunaendelea na uchunguzi juu yake,” alisem aKamanda Mungi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...