Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa leo Januari 27, 2016 amezindua kampeni ya upandaji miti Mkoani humo iliyofanyika katika Wilayaya ya Dodoma eneo la Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.
Kampeni hiyo imeshirikisha wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Dodoma, watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Dodoma, Wananchi na jumuiya ya chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, zoezi hili la upandaji miti litakuwa endelevu na litafanyika kwenye Wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma.
Katika uzinduzi huo, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameitaka kila Wilaya Mkoani humo kuhakikisha wanapanda miti isiyopungua Milioni moja na nusu (1.5 Mil.) na kuagiza viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa na kamati za mazingira za Vijiji, Miji na Mitaa kuhakikisha wanawasimamia wananchi kuhakikisha miti inapandwa maeneo ya Vilima, makazi, mashamba, kwenye shule na taasisi mbalimbali au maeneo maalumu yaliyotengwa.
Malengo ya kampeni ya upandaji miti mwaka huu Mkoani Dodoma ni kupanda jumla ya miti Milioni kumi (10 Mil.) lakini Mkuu wa Mkoa alibainisha kuwa changamoto kubwa inayokabili zoezi hilo ni uandaaji wa vitalu vya miche usio wa kutosha hivyo kutahadharisha kuwa inawezekana lengo la miti milioni kumi (10 Mil.) lisifikiwe na badala yake Mkoa ukafanikiwa kupanda miti milioni tano (5 Mil.).
Taarifa ya Manispaa ya Dodoma ambayo ndio mwenyeji wa uzinduzi wa kampeni za upandaji miti kwa Mkoa wa Dodoma mwaka huu, inaonesha kuwa, jumla ya miti 2500 itapandwa katika eneo la Hombolo ambapo miti 2000 itakuwa ya kivuli na miti 500 itakuwa ya matunda.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, mwaka jana zoezi la upandaji miti halikufanikiwa kutokana na uhaba wa mvua na pia changamoto nyingine inayochangia miti iliyopandwa kufa ni pamoja na ukame na baadhi ya miti kuliwa na mifugo.
Siku ya uzinduzi wa upandaji miti inafanyika Aprili Mosi kila mwaka, lakini kwa Mkoa wa Dodoma Mwezi Aprili ni mwisho wa mvua za masika, Hivyo, kutokana na hali hiyo, Mkoa wa Dodoma umeamua kuzindua upandaji miti Mwezi Januari ambapo mvua ni za kutosha.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa akipanda mti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti Mkoani humo iliyofanyika Hombolo Januari 27, 2016 na kushirikisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, watumishi wa umma na wananchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SACP. David Misime akipanda mti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti Mkoani humo iliyofanyika Hombolo Januari 27, 2016 na kushirikisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, watumishi wa umma na wananchi.
Baadhi ya Watumishi wa taasisi za Serikali Mkoani Dodoma kwa kushirikiana na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dodoma, wakishiriki uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti iliyofanyika Hombolo Dodoma Januari 27, 2016.
Baadhi ya Watumishi wa taasisi za Serikali Mkoani Dodoma kwa kushirikiana na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani humo na Wananchi, wakishiriki uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti iliyofanyika Hombolo Dodoma Januari 27, 2016
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa (kushoto) akitoa salamu zake wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti Mkoani humo iliyofanyika Hombolo Januari 27, 2016 na kushirikisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, baadhi ya watumishi wa taasisi za umma (pichani) na wananchi







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...