Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
MFANYABIASHARA Morris John au Maliyanga (46) na wenzake watatu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha wa vitu mbalimbali zikiwemo Dola za Marekani zenye thamani ya sh. milioni 18.5.
Maliyanga, mkazi wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, dereva pikipiki Frano Msaru au Singu (23) na wafanyabiashara Jeremiah Flavian (26) wakazi wa Sinza na Sandru Kamugisha (39), mkazi wa Kijitonyama, walifikishwa mahakamani hapo jana.
Washitakiwa walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, ambapo Wakili wa Serikali, Honolina Mushi, aliwasomea shitaka hilo.
Akiwasomea shitaka hilo, Honolina alidai washitakiwa walitenda kosa hilo, Desemba 22, mwaka jana, maeneo ya Mabibo Ruhanga, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Alidai kuwa siku hiyo washitakiwa hao waliiba Dola za Marekani 8,600 sawa na sh. milioni 18.5 fedha taslim sh. milioni 2.5, kompyuta mpakato, simu nne za mkononi mali ya Anderson Aloyce.
Inadaiwa kabla na baada ya kutenda kosa hilo, washitakiwa hao waliwatishia Zeno Genes, Aneth Paulo na John Renatus kwa bastola ili waweze kufanikisha kupata vitu hivyo.
Washitakiwa hao walikana shitaka hilo, ambapo Wakili Honolina alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Kwa upandewa mshitakiwa wa Msaru aliomba apewe kibali cha kwenda kutibiwa mguu kutokana na majeraha aliyodai kuyapata baada ya kupigwa akiwa polisi.
Aidha Hakimu alimtaarifu mshitakiwa huyo kwamba atapata matibabu na Jeshi la Magereza kwa kuwa wanatoa huduma hiyo.
Hakimu Hellen aliahirisha shauri hilo hadi Januari 27, mwaka huu kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kutokana na shitaka linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...