Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewaagiza Makandarasi
wa ujenzi wa barabara kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi kwa kuzingatia
haki, usawa na taaluma ya mtu kama ilivyoelekezwa kwenye sheria ya ajira hapa
nchini ili kuwezesha kazi za ujenzi kukamilika kwa wakati.
Amesema
hayo wilayani Chemba Mkoani Dodoma wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Dodoma-Babati
ambao ujenzi wake umegawanywa katika sehemu tatu ambazo Dodoma-Mayamaya Km.
43.65, Mayamaya-Mela Km. 99.35 na Mela-Bonga Km. 88.8 ili kuharakisha kasi ya kukamilika
kwake.
“Hakikisheni
leo hii mnawapa mikataba halali kwa mujibu wa taaluma zao na inayozingatia
sheria za Tanzania ili kujega uhusiano mwema wa kiutendaji na hivyo kazi zenu
zitakuwa na tija na ubora unaokusudiwa”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri
Mbarawa amekagua madaraja makubwa manne katika barabara hiyo ambayo ni Daraja
la Kelema lenye urefu wa mita 200, Msui lenye urefu wa mita 45, Kingali lenye
urefu wa mita 30, na Mela lenye urefu wa mita 30 na kuhimiza kasi ya ujenzi wa
madaraja hayo kabla ya mvua za masika.
Barabara
ya Dodoma-Babati ni sehemu ya Barabara Kuu ya Kaskazini (The Great North Road)
inayoanzia Cairo nchini Misri hadi Cape town Afrika Kusini.
“Barabara
hii ni kiungo muhimu cha miundombinu ya barabara za Tanzania kwani inaunganisha
mikoa maarufu ya kilimo ya nyanda za juu kusini, nyanda ya kati na nyanda ya
kaskazini na pia ni kiungo kikuu cha kwenda nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC)”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa
upande wake Eng. Deusdedit Kakoko kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS)
makao makuu, amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wamejipanga kuhakikisha
barabara hiyo ujenzi wake unakamilika kwa wakati ili kufungua fursa za kiuchumi
na kuunganisha kirahisi mkoa wa Dodoma, Manyara na Arusha.
“Mheshimiwa
Waziri tutaendelea kusimamia mradi huu umalizike kwa wakati na muda uliopangwa
na hatutaendelea kuvumilia wale wote wasioweza kumaliza mradi huu kwa wakati”,
amesisitiza Eng. Kakoko.
Waziri
Mbarawa amezungumzia umuhimu wa ubora wa barabara zinazojengwa na makandarasi
wote nchini kudumu kwa muda mrefu ili
thamani ya fedha inayotumika kuwalipa iwiane na huduma inayotolewa.
Hadi
sasa sehemu ya barabara ya Dodoma-Mayamaya (Km. 43.65), ujenzi wake umekamilika
kwa asilimia 80 wakati barabara ya Mayamaya-Mela (Km. 99.35), ujenzi wake umekamilika
kwa asilimia 52.2 na ujenzi wa barabara
Mela-Bonga (Km. 88.8), umekamilika kwa asilimia 45.17 ambapo ujenzi wa barabara
yote Dodoma-Babati unatarajiwa kukamilika baadaye mwakani.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano
Kazi ya ujenzi
wa mradi wa barabara ya Mayamaya-Mela yenye urefu wa Km. 99.35 ukiendelea.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akimuagiza Mkandarasi
wa mradi wa barabara ya Mayamaya-Mela kampuni ya China Henan International
Corporation Group Ltd (hayupo pichani) kuwapa mikataba bora ya kazi wafanyakazi
wanaojenga barabara hiyo (wanaomsikiliza).
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati) akiagiza
kuwekwa lami juu ya Daraja la Kola Wilayani Kondoa mkoani Dodoma ili kuanza
kupitika na kupunguza usumbufu wa magari wakati wa mvua. (kushoto) ni Meneja
ujenzi wa barabara ya Mela-Bonga (Km.88.8) Eng. Stone Cheng na (Kulia) ni
Mhandisi Mshauri wa barabara hiyo.
Mkandarasi
wa SynoHydo Corporation Ltd akimkabidhi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa barabara ya
Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa Km. 43.65 inaojengwa kwa kiwango cha lami
Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu akitoa
ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa
tatu kushoto) kuhusu hatua ya ujenzi iliyofikiwa katika barabara ya Mela-Bonga
(Km. 88.8) inayojengwa kwa kiwango cha lami, (Wa pili kulia) ni Mhandisi
Mshauri wa mradi huo Eng. Godfrey Kombe na (wa kwanza kushoto) ni Eng.
Deusdedit Kakoko kutoka TANROADS makao makuu.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...