Na  Bashir  Yakub. 
Mgawanyo  wa mali  za marehemu   hutegemea   mambo  makubwa  mawili. Kwanza  ni  ikiwa  marehemu  ameacha  wosia  na  pili  ni  ikiwa  hakuacha  wosia.  Ikiwa ameacha  wosia  basi  huwa ni rahisi  sana kwani mali  zake  zitagawanywa  kwa  kufuata  wosia.  Ikiwa  hakuacha  wosia  hapa  huwa  si  kwepesi  sana kwani  mali  zake  hulazimika  kugawanywa  kwa  mujibu  wa  sheria  zilizopo  wakati  sheria  zenyewe  ziko  tatu  tofauti. Wakati  mwingine ni  kazi  kidogo  kuamua  sheria  ipi  itumike  katika  kugawa  mali  za  marehemu. 

1.SHERIA  IPI  ITUMIKE  KATIKA  KUGAWA  MALI  ZA  MAREHEMU.
Ikiwa hakuna  wosia  swali  la  sheria  ipi  itumike  katika  kugawa  mali  za  marehemu  lazima  liibuke.  Kwa  ujumla  kuna  sheria  tatu  zinazotumika  katika  kugawa  mirathi.

( a )  Sheria  ya  kwanza  ni  sheria  ya  urithi  ya  India 1865 .  Hapa  kwetu  sheria  hii hujulikana  kwa  wengi  kama  sheria  ya  mirathi  ya  serikali. 

Sheria  hii  hutumika  kwa marehemu  ambaye hakuishi maisha  ya  kiislam  na hakuishi    maisha  ya  kimila. Zaidi  tunaweza  kusema  kuwa  sheria  hii  hutumika  kwa  wakristo  na  madhehebu  mengine  ambayo  sio   ya  kiislam.Hata  hivyo  hata  muislam  ambaye  itathibitika  kuwa hakuishi  maisha  ya  kiislam  wala  ya  kimila  sheria  hii itatumika  kugawa  mali  zake.

( b ) Pili  ni  sheria  ya kiislam.  Sheria  hii  hutumiwa  na waumini  wa  dini  ya  kiislamu. Lakini  haitoshi  kusema inatumiki  kwa  waislam  isipokuwa  inatosha  kusema itatumika kwa waliokuwa wakiishi  maisha  ya  kiislam. Sheria  hii  hufuata  misingi  ya  Quran  tukufu  na  Sunnah.

( c ) Tatu  ni  sheria  za  kimila. Sheria  hizi  hutumika  iwapo  marehemu  aliishi  maisha  ya  kimila. Mfano  wake  ni  kama  tunavyoona  kwa wamasai, wahadzabe,  na  makabila  mengine  hasa  vijijini  ambao huishi  maisha  yao  yote pasi  na  kufuata  dini  yoyote  isipokuwa  mila  tu. Sheria  hii  imo  katika  kanuni   za urithi,  tangazo  la  serikali  namba  436  la  mwaka  1963.

Kwa ujumla  swali  la   sheria  ipi  itumike   kugawa mali  za  marehemu  pale  ambapo  hakuacha  wosia,  hujibiwa  kwa   kuangalia  aina  ya  maisha  aliyoishi  marehemu. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...