Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Edda Sanga(katikati) akizungumzia mbele ya waandish wa habari (hawapo pichani) ni kwa jinsi gani wamepata malalamiko kutoka kwa familia zinazofanyiwa unyanyasaji wa kijinsia hasa ubakaji na ulawiti katika ngazi za mahakama, polisi na baadhi ya hospitali hapa nchini. 
Mratibu wa Kituo cha usuluishi cha TAMWA, Bi. Gladness Hemedi Munuo akizungumza mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati walipokuwa wakilaani vikali ucheleweshwaji na upotoshaji wa kesi za vitendo vya ukatili. 
Mwanasheria wa TAWLA, Mary Richard (wa kwanza kulia) akizungumza ni kwa jinsi gani wanavyowasaidia wanawake wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia leo katika mkutano na waandishi wa habari leo. 

CHAMA cha Wanahabari wanawake nchini Tanzania(TAMWA) kimelaani vikali ucheleweshwaji na upotoshwaji ushahidi wa kesi za vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji na ulawiti katika ngazi ya mahakama, polisi na baadhi ya madaktari hospitalini. Hali hiyo imekuja baada ya TAMWA kubaini kesi sitini na mbili (62) za ubakaji zimeshindwa kutolewa hukumu au uamuzi na mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2015. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Edda Sanga amesema kati ya kesi 63 za ubakaji, ni kesi moja tu mtuhumiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, kesi arobaini na tatu (43) bado ziko mahakamani, kesi kumi na saba (17) zimeshindwa kufika mahakamani ambapo kesi mbili zimefutwa kwa kukosa ushahidi. 

Pia aliongezea kwa kusema kuwa uongozi wa TAMWA umesikitishwa kuona kesi hizo zikicheleweshwa na vyombo mbalimbali vya serikali ikiwemo jeshi la polisi na mahakama. Na kuna baadhi ya viongozi wanapokea rushwa ili kuzima kesi za watoto wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia, pia baadhi ya polisi wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano kwa mlalamikaji ambapo wanatoa maneno ya vitisho na kupelekea mlalamikaji kukosa ujasiri wa kuhifadhi na kutetea kesi yake na wakati mwingine mama mzazi anaandikwa kama mlalamikaji badala ya mtoto mwenyewe aliyefanyiwa ukatili huo. 

Pia wameunga mkono tamko la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliposema wakati wa siku ya sheria duniani kuwa "Kila Hakimu wa Mahakama anapaswa kuhukumu kesi si chini ya 260 kwa kila mwaka na kwa haki", Hivyo basi wao kama TAMWA wanaamini ndani ya mwaka huu Mahakama hapa nchini zitafanya kazi yao kiweledi ili kuweza kupunguza ukatili wanaofanyiwa watoto wa kike.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. TAMWA tafadhari msichoke wala msije mkakata tama, tuna hakika shetani atalegea tu.
    Poleni sana ndugu wa watoto na wanawake waliofikwa na haya matendo ya kinyama katika jamii yetu.
    Idara tatu, yaani Mahakama zote, Polisi na Takukuru ni idara zenye uvundo sana. Idara hizi tatu zinahitaji kufumuliwa toka juu hadi chini na kusukwa upya. Hasa hasa mahakama huko kuna MUNGU WATU.
    Mheshimiwa raisi, waziri mkuu na mawaziri husika wa idara hizi tatu fanyeni dharula. Eleweni kwamba bila hizi idara tatu kuwa safi basi idara zingine kama maji, umeme, aridhi, madini, wanayma pori nk itakuwa ngumu kusafishika.
    Je, watoto wa watumishi wa mahakama na Polisi wakibakwa ndiyo haki itatolewa?
    Fanyeni hima. Wala msimtizame nyani usoni.
    Poleni sana wote mulioumizwa

    ReplyDelete
  2. Rais aliongea viongozi wa siasa wakaleta siasa kama kawaida yao wakasema ameingilia uhuru wa mahakama. Sasa sikia hivyo vilio..mtasema tamwa wameingilia uhuru wa mahakama.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...