Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali inatarajia kutekeleza zoezi la utozaji faini kwa wamiliki waliobadili matumizi ya ardhi kinyume cha sheria kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Denis Rugemalila wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango kazi wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Akifafanua kuhusu zoezi hilo Bw. Rugemalila amesema kuwa kuanzia Februari 8, 2016 Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Temeke, Kinondoni na Ilala itaanza operesheni jijini Dar es Salaam ya kukagua na kutoa adhabu ikiwemo kutozwa faini kwa waendelezaji wote waliobadili matumizi ya Ardhi na kuongeza majengo kinyume cha sheria.
Aidha Bw. Rugemalila ameeleza kuwa licha ya tozo za faini hatua nyingine stahiki zitachukuliwa dhidi ya maendelezo ya ardhi ambayo yamefanyika bila vibali kama vile viwanda, vituo vya mafuta na shughuli nyingine zinazoathiri mazingira na kuleta kero kwa jamii.
“Endapo kutabainika kuwepo kwa vibali vinavyotia mashaka, vitaainishwa ili vifanyiwe uhakiki kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.” Alisema Rugemalila.
Sanjari na zoezi hilo pia wizara ya Ardhi inaendelea na zoezi la usambazaji wa hati za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi na watakaokaidi watafikishwa mahakamani pamoja na kushika mali zao, kufilisi au kufutiwa kwa miliki zao.
“Tunawaomba wamiliki wote wa ardhi nchini kulipa kodi ya pango la ardhi na kutoa ushirikiano kwa maafisa wetu watakapokuwa wanapita kufanya ukaguzi” alisema Rugemalila.
Serikali imeamua kuendesha zoezi la utozaji faini baada ya kubaini kuwa kuna baadhi ya waendelezaji wa ardhi wamekuwa wakibadili matumizi ya ardhi kiholela na kusababisha kero kwa umma, pia baadhi ya waendelezaji wanaongeza majengo tofauti na yale yaliyoidhinishwa kujengwa katika kiwanja husika.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Denis Rugemalila akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu mpango kazi wa utekelezaji wa mkakati wa utozaji faini kwa wamiliki waliobadili matumizi ya ardhi kinyume cha sheria. Kushoto ni Afisa Sheria Mwandamizi Bi. Martha Isaga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...