Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Wawekezaji kutoka  katika makampuni yanayojihusisha na uzalishaji wa nishati ya umeme kutoka nchini China, wameeleza nia ya kuwekeza kwenye  sekta ya nishati  nchini  ili iweze kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Waliyasema hayo katika kikao na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo pamoja na wataalam kutoka  Wizara ya Nishati na Madini  pamoja na  taasisi  mbalimbali ikiwa ni pamoja  na Shirika la  Umeme Nchini (TANESCO), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)

Akizungumza katika kikao hicho Mwakilishi kutoka Umoja wa Wafanyabiashara katika Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Lin Zhiyong, alisema kuwa nia ya makampuni yanayojishughulisha na  uzalishaji wa nishati ya umeme ni kubaini fursa zilizopo katika sekta ya nishati nchini kabla ya kuja kuwekeza rasmi

Aliongeza kuwa  ujumbe maalum wa wawekezaji kutoka   nchini  China unatarajiwa kuwasili nchini mapema wiki ijayo kwa ajili  ya kupata  taarifa mbalimbali zenye kubainisha  fursa za uwekezaji nchini  ikiwa ni pamoja na mpango  kabambe (master plan), sera, na mpango mkakati katika sekta ya nishati, kabla ya kusaini makubaliano ya awali kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya  umeme.

Zhiyong  alisisitiza kuwa wawekezaji  kutoka China wako   tayari kushirikiana na wawekezaji wa ndani  ya  nchi kwenye uzalishaji wa nishati ya umeme  ili  taifa liweze kupata  nishati ya uhakika kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini  anayeshughulikia nishati Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo alishukuru ujumbe  huo na kueleza kuwa  fursa za uwekezaji  kwenye  sekta ya nishati ni nyingi na kuwataka kuchangamkia fursa hizo.

“Wananchi wanahitaji nishati ya  uhakika ambayo ni kichocheo cha  ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo tunawakaribisha kuwekeza katika uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kuwa  tuna vyanzo  vingi kama  vile  gesi, jotoardhi, makaa ya mawe, jua, upepo n.k,” alisisitiza Dk. Palangyo.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini  anayeshughulikia nishati Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akisalimiana na mmoja wa wajumbe  kutoka kampuni  uzalishaji wa makaa ya mawe ya  Shenhua Ningxia Group Co. Limited kutoka China. (kushoto). Katikati ni Mwakilishi kutoka Umoja wa Wafanyabiashara katika Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Lin Zhiyong.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia nishati, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akielezea fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati nchini. Kushoto ni Mwakilishi kutoka  Umoja wa Wafanyabiashara katika Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Lin Zhiyong.
 Sehemu ya ujumbe kutoka nchini China ukifuatilia majadiliano mbalimbali  yaliyokuwa yanaendelea katika kikao hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...