Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa (katikati) akizungumza na Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Vietnam Bw. Nguyen Bac Son (kushoto) kuhusu ushirikiano baina ya Tanzania na Vietnam na (kulia) ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwini Ngonyani.
Waziri wa Habari na
Mawasiliano wa Vietnam Bw. Nguyen Bac
Son (kulia) akimuaga mwenyeji wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mhe. Profesa Makame Mbarawa wa pili (kushoto) baada ya kufanya mazungumzo ya
ushirikiano katika sekta ya Mawasiliano, (kushoto) ni Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwini Ngonyani.
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
VIETNAM
KUPANUA WIGO WA UWEKEZAJI KWENYE SEKTA YA MAWASILIANO TANZANIA.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (Mb) amekutana na
Waziri wa Habari na Mawasiliano wa nchi ya Vietnam Bwana Nguyen Bac Son ofisini
kwake kwa lengo la kupanua wigo wa uwekezaji kwenye Sekta ya Mawasiliano nchini
Tanzania na kushirikiana kwa pamoja kuendeleza Sekta hizo baina ya Tanzania na Vietnman.
Kikao hicho ni muendelezo wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti wa Vietnam,
Mhe. Truong Tan Sang na ujumbe wake nchini Tanzania.
Prof.
Mbarawa alisema kuwa Tanzania imekuwa na ushirikiano na Vietnam kupitia Kampuni
ya Viettel kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya kufikisha huduma za mawasiliano
vijiini kwa kutiliana saini Mkataba. Mkataba huo ni wa miaka mitatu kuanzia
mwezi Oktoba mwaka 2014 hadi Novemba, 2017 ikijumuisha ujenzi wa miundombinu ya
Mkongo wenye urefu wa kilomita 20,000 kwenye wilaya zote nchini; kujenga
miundombinu ya mawasiliano kwenye vijiji
4,000; kuunganisha Ofisi za Wakuu wa Wilaya; hospitali za Wilaya; Ofisi
zote za Posta za Wilaya; na kupeleka na
kutoa huduma za intaneti bila malipo kwenye shule 3 za Sekondari za Serikali
katika kila Wilaya nchini kwa kipindi cha miaka mitatu.
Aidha,
Prof. Mbarawa aliongeza kuwa tangu Kampuni ya Viettel yenye jina la biashara la
Halotel ilipoanza kufanya kazi rasmi mwezi Oktoba mwaka 2015, imeweza kupeleka
huduma ya mawasiliano maeneo ya vijijini na hadi hivi sasa ina watumiaji wa
simu za mkononi wapatao milioni 1.2 na wananchi walio wengi wanafurahia huduma
hiyo tofauti na hali ilivyo kuwa hapo awali kipindi cha miezi sita iliyopita na
ikizingatiwa kuwa sehemu nyingine za vijijini hapakuwa na mawasiliano. Pia
alisema kuwa, “Serikali ya Tanzania itaendelea kujenga na kuwekeza kwenye Sekta
ya Mawasiliano ili kuwavutia wawekezaji na kampuni za simu za mkononi ambapo
Serikali ya Tanzania ilitoa ruzuku kiasi cha dola za marekani milioni 30 ili
kuziwezesha kampuni hizo kupeleka mawasiliano vijijini na maeneo yasiyokuwa na
mvuto wa kibiashara”. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016 Halotel imejenga Mkongo
wenye urefu wa kilomita 18,000 kati ya kilimota 20,000; na kujenga miundombinu
ya mawasiliano kwenye vijijini 1,605 kati ya vijiji 4,000 visivyokuwa na
mawasiliano.
Katika
mazungumzo hayo ya kuendeleza sekta ya Mawasiliano Tanzania, Prof. Mbarawa
aliwaalika wawekezaji kutoka Vietnam wa Sekta ya Mawasiliano na kampuni ya
Halotel kujiandaa na kuja Tanzania kushiriki mnada wa kununua masafa ya 700MHz ambayo
yamepatikana baada ya kuhama kutoka Teknolojia ya Utangazaji ya Analojia na
kuhamia Teknolojia ya Utangazaji ya Dijitali.
Pia alisema kuwa Kampuni za Vietnam zinakaribishwa kuanzisha na
kuendeleza huduma za mawasiliano za mfumo wa kumpatia mteja huduma tatu kwa
pamoja ya sauti; intaneti; na kuangalia televisheni ikijulikana kwa jina la triple player ili Tanzania iweze kwenda
sambamba na kasi ya ukuaji wan a maendeleo ya TEHAMA yanayotokea dunia nzima.
Katika
kikao hicho, Prof. Mbarawa alimweleza Mhe. Ngoyen Bac Son kuwa Tanzania iko
tayari kusaini Mkataba wa Makubaliano ya ushirikiano na Serikali ya Vietnam wa
kubadilishana wataalamu kwenye Sekta ya Mawasiliano na kuwapatia mafunzo ili
kujenga uwezo wa wataalamu wetu wa Tanzania; na kuanzisha na kuendeleza viwanda
vidogo vidogo vya TEHAMA (ICT Small Scale Factories) nchini Tanzania ambapo
viwanda hivyo vitazalisha ajira; kurahisisha upatikanaji wa vifaa na huduma za
TEHAMA kuendana na mahitaji na mazingira yetu; kuongeza mapato; na kuwahudumia
wateja wa nchi za jirani na Tanzania.
Mhe.
Ngoyen Bac Son alisema kuwa Serikali ya Vietnam iko tayari kuendeleza
ushirikiano baina ya Serikali yao na ya Tanzania ya kuendeleza Sekta ya
Mawasiliano; na sekta ya kukuza Uchumi
na Maendeleo ya Tanzania kama alivyozungumza Rais wa Vietnam. Pia aliongeza
kuwa, “Serikali ya Vietnam iko tayari kuleta kampuni za kuwekeza Tanzania kwa
kuanzisha Kiwanda cha vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya kuwapatia watanzania
huduma za mawasliano na ni matarajio yetu kuhakikisha kuwa ni kiwanda kikubwa
ambacho kitahudumia na wateja wa nchi za jirani na Tanzania”. Aidha, Mhe.
Ngoyen Bac Son aliongeza kuwa Serikali ya Vietnam inaridhia kusaini Mktaba wa
Ushirikiano baina ya nchi hizo na amewakaribisha wafanyabiashara na kampuni za Tanzania
kwenda kuwekeza nchini Vietnam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...