Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeiagiza serikali kuwachukulia hatua kali wale wote waliovamia miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na kuigeuza kuwa masoko ya bidhaa zao.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Jasson Rweikiza amesema hali hiyo haivumiliki na inapaswa kukomeshwa mara moja. Kamati hiyo ilkutana kwa mara ya pili na uongozi wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) jana jijini Dar es Salaam.
“Tumejionea katika ziara yetu tuliyoifanya katika miundombinu ya mradi kuwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wameivamia miundombinu na kuigeuza kuwa masoko,” alisema Bw. Rweikiza.
Bw. Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini alisema jambo hilo haliwezi kufumbiwa macho kwani maradi huo umeghalimu fedha nyingi na zitalipwa na kodi ya watanzania.
Alisema pia baadhi ya madereva wa magari na pikipiki maarufu kama bodaboda wameharibu baadhi ya miundombinu na kwamba wanatakiwa kudhibitiwa. Aliitaka serikali kuweka ulinzi na wote wanaobainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Aliutaka uongozi wa Wakala wa DART kuipatia majibu kamati yake kulingana na maswali waliyouliza ifikapo tarehe 4 mwezi wa Nne.
Kamati ilitaka kujua miongoni mwa mambo mengine swala la nauli za mabasi, tarehe ya kuanza kwa mradi, na mkataba kati ya DART na mtoa huduma wa mpito wa mradi.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART, Bw. Ronald Lwakatare alisema Wakala umejipanga kutoa majibu kwa kamati ya Bunge kwa wakati ili kuiwezesha kuzifahamu kazi za wakala na changamoto zilizopo.
“Tunazo changamoto nyingi zikiwemo za ofisi, uchache wa wafanyakazi, ufinyu wa bajeti, uharibifu wa miundombinu na mengine,”alisema.
Alisema kamati hiyo, serikali na wakala zinatakiwa kuwa karibu ili awamu ya kwanza ya mradi iweze kukamilika nakuanza na awamu nyingine zianze.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Suleiman Jaffo aliwataka wananchi kuendelea kuwa na subira na kuahidi kuwa mradi huo utaanza hivi karibuni na kutoa huduma nzuri ya usafiri.
“Kuna mambo yanakamilishwa ndani ya serikali na wadau wake yakiwemo kufunga mfumo wa utozaji nauli kwa njia ya kadi na mengine,” alisema waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Kisarawe.
Alisema nauli zitakazotozwa katika mradi huo zitakuwa rafiki kwa wananchi hivyo wasiwe na wasiwasi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Suleiman Jaffo akisisitiza jambo kwa wajumbe wa kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na uongozi wa wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) jijini Dar es Salaam jana. kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Jasson Rweikiza na Kaimu Afisa Mtendaji wa Wakala, Bw. Ronald Lwakatare (kulia). Kamati hiyo ilikutana na uongozi wa wakala huo kuzungumzia mambo mbalimbali ya kuhusu mradi huo.
Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Bw. Jasson Rweikiza akisisitiza jambo kwa wajumbe wa kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na uongozi wa wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) jijini Dar es Salaam jana. Kamati hiyo ilikutana na uongozi wa wakala huo kuzungumzia mambo mbalimbali ya kuhusu mradi huo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Ronald Lwakatare akisisitiza jambo kwa wajumbe wa kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na viongozi wa wakala huo jijini Dar es Salaam jana. Kamati hiyo ilikutana na uongozi wa wakala kuzungumzia mambo mbalimbali ya kuhusu mradi huo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...