Katika jitihada za kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
inafikia viwango vya kimataifa kulingana na matakwa ya Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO), Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kimefanikiwa kufanya awamu
ya tatu ya kozi ya huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa anga kwa baadhi ya
wafanyakazi wa TMA.
Akifunga rasmi kozi hiyo na kuwatunuku vyeti wahitimu, Mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi aliwataka wahitimu wote pamoja na
wafanyakazi wengine wa Mamlaka kuwa vielelezo katika vituo vyao vya kazi
katika kuzingatia maadili, kanuni na taratibu za kazi na kufanya kazi kwa weledi
mkubwa hususani kwenye sekta ya usafiri wa anga. Aidha aliahidi kwamba Bodi
itashirikiana na menejimenti ya TMA kuhakikisha kwamba miundo mbinu ya
Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma inaboreshwa.
Akimkaribisha mgeni rasmi Dkt. Agnes Kijazi, Mkuruggenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Hali ya Hewa alisema mafunzo hayo ni sehemu ya kutekeleza mpango mkakati
wa Mamlaka wa kuendeleza watumishi ili kukidhi viwango vya Shirika la Hali ya
Hewa Duniani.
Naye Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma, Bw. Joseph Aliba alitoa shukrani
za dhati kwa serikali kwa kuwezesha uboreshaji wa huduma kama vile usajili wa
chuo, maktaba, ujenzi wa uzio wa chuo, mafunzo kwa waalimu, kuunganishwa
katika mkongo wa Taifa huku akitaja baadhi ya changamoto zilizopo.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wote, Bi. Beatrice Kitero, alishukuru
Mamlaka kwa mafunzo na kuahidi kuyafanyia kazi katika uboreshaji wa huduma
za hali ya hewa kwaajili ya usafiri wa anga nchini.
Kozi ya huduma za hali ya hewa kwaajili ya usafiri wa anga, imeandaliwa na
Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kwa muda wa mwezi mmoja na ilifanyika
Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Dar es Salaam. Wahitimu ni wafanyakazi
wa Mamlaka waliohitimu degree ya Hali ya Hewa kutoka vituo vya Mbeya,
Dodoma, Kigoma, Makao Makuu (DSM) na Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...