WANANCHI wa Jimbo la
Kikwajuni Zanzibar, wametakiwa kujenga tabia ya kufanya usafi wa mazingira
katika maeneo yao ili kuepuka maradhi ya kipindupindu yanayoathiri maeneo mbali
mbali nchini.
Wito huo umetolewa kwa
nyakati tofauti na Mbunge wa jimbo la Kikwajuni, Muandisi Hamad Yussuf Masauni
alipokuwa akifanya usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo
Mjini hapa.
Alisema maeneo mengi ya
jimbo hilo hasa katika Majumba ya Maendeleo ya Michenzani ni machafu sana hali inayoweza kusababisha maradhi ya miripuko
yakiwemo kipindupindu na kichocho.
Masauni ambaye pia ni
Naibu Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, alieleza kuwa wananchi wa maeneo hayo
wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira na kupelekea
uharibifu wa miundombinu ya kusafirisha maji taka ikiwemo mitaro kuziba.
“ Nachukua fursa hii
kuwakumbusha wananchi wa kikwajuni kuwa suala la usafi wa mazingira halina
itikadi za kisiasa ni lazima wananchi sote tuungane bila ya kujali tofauti za
kisiasa.
Pia nakuombeni wananchi
hasa mnaoishi katika majumba ya michenzani mbadilike kwa kujali mazingira yenu
kwani mjue kuwa endapo eneo hili litapata maradhi ya mripuko kuna hatari ya
wananchi wengi kupoteza maisha kwa maradhi ambayo tuna uwezo wa kuyazuia.”,
alisema Masauni huku akisisitiza umuhimu wa kufanya usafi wa mara kwa mara katika
maeneo hayo.
Alisema viongozi wa
jimbo hilo kwa sasa wanapanga kuanzisha kikundi maalum cha vijana wa kufanya
usafi katika maeneo ya jimbo hilo, ambapo kila kaya(nyumba) watakuwa
wanachangia kiasi cha shilingi 200 kila siku ili fedha hizo ziweze kuwasaidia
watu wanaofanya usafi huo.
“Aibu kubwa kuona ndani ya jimbo la kikwajuni
panaanza kupatikana wagonjwa wa maradhi ya kipindupindu kwani ni jimbo lenye
sifa ya usafi na ukaribmu toka enzi na enzi tena lipo mjini, lazima
tushirikiane kufanya usafi katika maeneo yetu.” Alisema Masauni.
Aidha aliishauri
Manispaa ya Zanzibar kuanza mara moja utafti wa kubaini mifumo ya maji machafu
na masafi inayoingiliana katika maeneo hayo ili kuifanyia matengenezo kwa
haraka kabla hapajatokea maafa ya maradhi ya miripuko na kusababisha athari kwa
wananchi wa maeneo hayo.
Kwa upande wake
Mwakilishi wa Jimbo hilo, Nassor Salum Ali(Jazeera) aliwapongeza wananchi wa
jimbo hilo waliojitokeza kufanya usafi wa mazingira kwa lengo la kuweka maeneo
yako katika hali ya usafi.
Jazeera alisema kwamba
kinga ya maradhi ya mripuko hasa kipindupindu ni usafi wa mazingira hivyo kila
mwananchi anatakiwa kutekeleza wajibu wake bila ya kulazishwa na mtu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...