JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
Matukio ya ubakaji hasa
kwa watoto wadogo yamekuwa yakiongezeka kwa kiwango kikubwa, ongezeko hili
limebainika kutokana na ufuatiliaji tulioufanya kupitia matukio yaliyoripotiwa katika
vituo vya Polisi ambapo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2016
kumeripotiwa matukio 1765 ukilinganisha na matukio 1585 katika kipindi kama
hicho mwaka 2015 ikiwa ni ongezeko la matukio 180.
Katika matukio ya Januari hadi machi 2016, jumla
ya watuhumiwa 823 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ingawa bado kumekuwa na
tabia ya wazazi na walezi kuficha watuhumiwa wa ubakaji na kumaliza kesi hizo kirafiki au kifamilia
jambo ambalo ni kinyume cha sheria bila kuzingatia madhara aliyoyapata mtoto.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linakemea
vikali wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu vya ubakaji na wazazi
ama walezi wanaofumbia macho vitendo hivyo na kuingia makubalino na watuhumiwa
kwa kupeana fedha kama fidia ili wamalize kesi kiundugu au kifamilia.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa Wazazi, walezi, Viongozi wa dini, Asasi za
kiraia, walimu na Wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano katika
kushughulikia vitendo hivyo ikiwemo kuwafichua wazazi au walezi wanaofanya
makubaliano ya kumaliza kesi za ubakaji kirafiki au kifamilia ili kukomesha
vitendo hivyo.
Imetolewa na:
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu
ya Polisi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...