Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO
Serikali inaendelea
kufanya kazi kwa ushirikiano na wanahabari nchini ili kuhakikisha wananchi
wanapata taarifa mbalimbali zinazofanywa na Serikali yao katika nyanja za
kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ili kuhakikisha Watanzania wanafikia maendeleo
yao na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa
na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye alipokuwa
akichangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini
Dodoma.
“Waandishi wa habari
wapo huru kuuliza maswali kwa Wabunge na kuandika habari kupitia vyombo vyao na
kuwapatia wananchi taarifa mbalimbali zinazoendelea bungeni” alisema Waziri
Nape.
Kuhusu idadi ya
vyombo vya habari nchini, Waziri Nape amesema kuwa Tanzania ni nchi yenye
vyombo vingi vya habari yakiwemo magazeti, redio na televisheni ambavyo ni
ishara wazi kuwa vyombo hivyo vipo huru kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili
ya taaluma ya tasnia ya habari pamoja na katiba, Sheria, kanuni na taratibu za
nchi.
Waziri huyo alisema
kuwa Tanzania sio nchi ya kwanza kutokurusha matangazo ya bunge moja kwa moja
(live), utaratibu huo unafuatwa na Mabunge yote ya jumuiya ya Madola.
Waziri Nape amesema
kuwa bado Serikali inakusudia kuboresha mazingira ya waandishi wa habari ili
waweze kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru hasa wanapotimiza majukumu yao ya
kiundishi wa habari.
Aidha, amewashukuru
wabunge kwa uzalendo wao wa kubaki ndani ya bunge na kujadili masuala
mbalimbali ya maendeleo ya nchi yao kwa manufaa ya wananchi wanaowawakilisha.
Kwa upande wake
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Gorge Masaju amewashukuru wabunge kutimiza haki
yao ya Kikatiba kuingia Bungeni na kushiriki mijadala mbalimbali kulingana na
ratiba iliyopo
Kwa mujibu wa ibara
ya 63 (2),
Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na
madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kuhusu matangazo ya
Bunge kurushwa moja kwa moja, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Masaju alisema kuwa
Watanzania wanaendelea kupata taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari
nchini.
Kwa mujibu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara 18. (2) Kila raia anayo haki ya kupewa
taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni
muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa
jamii.
Akitoa ufafanuzi wa
ibara hiyo Masaju alisema kuwa haki ya kupewa taarifa, siyo haki ya kuonekana na
vile vile maamuzi ya Bunge hayafanywi kwa muonekano, bali hufanywa kwa majadiliano
ya Wabunge wakiwa Bungeni.
Bunge litaendelea na vikao
vyake Jumatano Aprili 27, baada ya kuahirishwa kwa mapumziko ya maadhimisho ya
Sherehe za miaka 52 ya Muungano wa Tanzania na ambapo mwaka huu Watanzania wametakiwa
kuiadhimisha wakiwa majumbani au wakiwa katika shughuli zao binafsi.
Mapema mwezi huu Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alielekeza fedha zilizopangwa
kutumika katika maadhimisho hayo ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 2 za
Tanzania zitumike kupanua barabara ya Mwanza Airport katika eneo linaloanzia
Ghana Quarters hadi uwanja wa ndege wa Mwanza ili kupunguza adha ya msongamono wa
magari katika barabara hiyo Jijini humo.
Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Dkt. Possy
Abdallah akichangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni
mjini Dodoma na kusisitiza juu ya Serikali inavyosimamia suala la watu wenye
ulemavu nchini. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira Walemavu Jenista Muhagama na kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo
Anthony Mavunde.
Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Mpango (aliyesimama) akichangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri
Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini Dodoma na kusisitiza Wizara yake inavyochangia
masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii nchini.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye akichangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri
Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini Dodoma na kusisitiza kuwa Serikali
inaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wanahabari nchini.
Wabunge wakifuatilia
mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini
Dodoma. (Picha na Eleuteri
Mangi-MAELEZO)






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...