Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng.Joseph
Nyamhanga ametambulisha utaratibu mpya utakaotumika kupunguza vikwazo visivyo
vya kiforodha ili kurahisisha biashara na usafirishaji kwa magari makubwa yanayosafiri
kwenda nje ya nchi.
Utaratibu huo unaotarajiwa kuanza Mei mwaka huu utawezesha magari yanayosafiri nje
ya nchi kukagulia katika vituo visivyozidi vinne ili kupunguza muda wa safari kwa magari
yaendayo nje ya nchi na kuvutia wasafirishaji kutumia bandari ya Dar es Salaam.
“Tumetayarisha stika zitakazobandikwa kwenye magari yanayokwenda nje ya nchi
ambayo yatasimama na kukaguliwa katika vituo vitatu kwa magari yanayotumia
barabara ya kanda ya kati na vinne kwa yanayotumia kanda ya Dar es salaam yaani
TANZAM ”amesema Eng. Nyamhanga.
Eng. Nyamhanga amevitaja vituo hivyo vya barabara ya ukanda wa kati kuwa ni
Vigwaza mkoani Pwani, Manyoni mkoani Singida na Nyakanazi mkoani Kagera na kwa
ukanda wa Dar es salaam yaani barabara kuu ya TANZAM- Dar es salaam hadi
Tunduma na Uyole hadi Kasumulu vitatumika vituo vine ambavyo ni Vigwaza mkoani
Pwani,Mikumi mkoani Morogoro, Makambako mkoani Njombe na Mpemba mkoani
Songwe.
Vituo hivyo vya ukaguzi wa pamoja vitakuwa na huduma ya Mizani, Vituo vya Polisi,
Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), na maeneo ya kupumzikia madereva
wanaosafiri kwenda nje ya nchi.
Katika hatua nyingine Eng. Nyamhanga amesema ili kurahisisha biashara ya usafirishaji
kati ya Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Africa (SADC), na Jumuiya ya Soko la Pamoja kwa Nchi za Mashariki na
Kusini mwa Afrika (COMESA) Serikali inaendelea kutoa huduma za pamoja mipakani
one stop border post inayolenga kurahisisha huduma za forodha,uhamiaji na usimamizi
wa ubora wa bidhaa na huduma ,ulinzi na usalama kwa kutoa huduma hizo upande
mmoja wa mpaka kwa nchi mbili husika.
Vituo hivyo vinavyojengwa katika mipaka ya Holili, Namanga, Horohoro,Sirari, Mtukula,
Rusumo, Kabanga, Tunduma na Kasumulu vitaimarisha huduma za forodha,uhamiaji
ulinzi na usalama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Eng.
Joseph Nyamhanga, akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika
uzinduzi wa stika za upimaji uzito katika mizani kwa magari makubwa yanayosafiri
kwenda nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Eng.
Joseph Nyamhanga, akitoa ufafanuzi kuhusu stika za upimaji uzito katika mizani kwa
magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...