STATE HOUSE
ZANZIBAR.
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19.4.2016.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ameeleza kuwa juhudi za makusudi sambamba na mashirikiano ya pamoja zinahitajika
katika kupambana na maradhi ya kipindupindu ambayo yameonesha kushika kasi hivi
sasa hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo katika mazungumzo
kati yake na uongozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa Tanzania, ukiongozwa
na Mwakilishi wa Shirika hilo Dk. Chatora Rufaro pamoja na viongozi wengine wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) wanaofanya kazi zao hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliyapongeza
mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayofanya kazi zake hapa nchini likiwemo Shirika
la Afya Duniani (WHO), pamoja na UNICEF katika juhudi zao za kuendelea kuiunga
mkono Zanzibar hasa katika mapambano ya maradhi ya kipindupindu yalioibuka hivi
sasa.
Dk. Shein alisema kuwa ujio wa Mwakilishi
huyo wa (WHO) hapa nchini katika kipindi hichi ni muhimu sana na utasaidia kwa
kiasi kikubwa katika kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
Wizara ya Afya katika kusaidia mapambano ya maradhi hayo.
Alisema kuwa iwapo juhudi za makusudi
zitachukuliwa na kila mmoja akafanya wajibu wake ipasavyo sambamba na kuwa na mwamko katika kuchukua tahadhari kuhusu
kujikinga na maradhi ya kipindupindu hatua hiyo itasaidia katika
kupambana na maradhi hayo ambayo hatimae yatapungua ama kuondoka kabisa.
Dk. Shein alisema kuwa maradhi hayo yana
historia hapa Zanzibar na yaliwahi kuibuka katika miaka ya nyuma lakini baada
ya juhudi kubwa za kuyatokomeza kuchukuliwa na Serikali kwa mashirikiano na
wananchi pamoja na washirika wa maendeleo yalichukua muda kuibuka tena kutokana
na juhudi za pamoja zilizochukuliwa wakati huo.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya
kudumisha usafi hasa katika maeneo yote ya visiwa vya Zanzibar yakiwemo maeneo
ya Manispaa ya mji wa Zanzibar ambayo hali ya usafi wa mji huo haiko vizuri
hali ambayo inachangia kuibuka kwa maradhi hayo.
Akieleza umuhimu wa kutumia dawa za kutia
kwenye maji yaani vidonge vya “water guard” Dk. Shein alisema kuwa mbali ya
hatua hiyo watendaji wa Wizara ya Afya nao wanajukumu kubwa katika kutekeleza
majukumu yao na kusisitiza ulazimu wa kutumia maadili yao ya kazi katika kuwasidia
wananchi.
Akigusia suala zima la elimu kwa jamii,
Dk. Shein aliitaka Wizara ya Afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi mara kwa
mara kupitia vyombo vya habari juu ya athari, kinga na maambukizi ya maradhi
hayo.
Dk. Shein alisema kuwa mripuko wa maradhi
hayo katika kipindi hichi ni changamoto kubwa kwa Wizara ya Afya na kueleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuzisaidia
sekta zote katika kupambana na maradhi hayo.
“Maradhi
ya kipindupindu ni rahisi kupambana nayo iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake
na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia maji
yasiyo salama ambayo ni moja ya chanzo kikubwa cha kupata maradhi haya….. kama
tulivyofanikiwa kupambana na Malaria nalo hili linawezekana”,alisema Dk. Shein.
Nae
Mwakilishi wa (WHO) nchini Tanzania Dk. Rufaro Chatora alimueleza Dk. Shein
azma ya Shirika hilo katika kuisaidia Zanzibar kwenye vita ya kupambana na
maradhi hayo hapa nchini na kusisitiza umuhimu wa kuwepo mashirikiano na
uratibu wa pamoja kati ya taasisi za Serikali, taasisi za kiraia na watu
binafsi katika kutekeleza wajibu wao juu ya kukabiliana na kipindupindu.
Mwakilishi
huyo alieleza kuwa tokea mwezi wa Septemba mwaka jana yalipoibuka maradhi hayo
hapa Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Afya na kuahidi
ushirikiano zaidi katika kupambana na tatizo hilo huku akisisitiza haja kwa
vyombo vya habari kusaidia juhudi hizo.
Aidha,
Mwakilishi huyo wa (WHO) amesema kuwa Shirika hilo kwa kushirikiana na
mashirika mengine ya Kimataifa litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maradhi hayo ili kuhakikisha
yanamalizika.
Sambamba
na hayo, kiongozi huyo alieleza kuwa chanzo kikubwa cha maradhi hayo ni maji
hivyo kuna kila sababu ya kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kutumia maji
yalio safi na salama ikiwa ni pamoja na kutumia ‘water guard’ pamoja na
kuimarisha usafi katika maeneo yote.
Akizitaja
tahadhari juu ya maradhi hayo, Dk. Chatora alisema ni pamoja na kuweka
mazingira safi, kufuata masharti ya afya, kuchemsha maji ya kunywa ama kutumia
maji yaliyotiwa dawa ya kuulia bektiria wanaosababisha maradhi ya kipindupindu.
Pia,
Mwakilishi huyo alieleza haja kwa wananchi
kuwapeleka mapema katika vituo vya afya watu wanaobainika na dalili za maradhi
ya kipindupindu kwa vile imeonekana wagonjwa wengi wanapopelekwa vituoni afya
zao zinakuwa mbaya na hatimae matibabu yanakuwa magumu.
Mapema aliekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk.
Mohammed Saleh Jidawi alieleza mashirikiano na uhusiano mwema uliopo kati ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo (WHO)
jinsi linavyotoa ushirikiano wake katika vita ya kupambana na maradi hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...