Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto inalaani vikali tukio La mauaji ya mtoto
wa kike, umri miaka 9, ambaye alininajisiwa kwa zamu na watu wasiojulikana, na hatimaye kumkata
mapanga yaliyosababisha kuuawa kwa mtoto huyo mdogo, katika kijiji cha Kapanga, wilaya ya
Sumbawanga mkoani Rukwa.
Wizara imepokea kwa huzuni kubwa taarifa kuhusu mazingira ya mauaji ya mtoto huyo, ambaye
alifanyiwa ukatili mkubwa yaliyosababisha kifo cha mtoto huyo katika umri mdogo.
Wizara inapongeza agizo la Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima, ambaye amelitaka jeshi la
polisi wilayani Sumbawanga kuhakikisha wanawasaka na kuwatia mbaroni watuhumiwa wa mauaji ya
mtoto ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika, na hivyo kuwa fundisho kwa watu
wengine.
Wizara inapongeza ushirikiano uliooneshwa na wakazi wa kijiji cha Kapanga wilayani Sumbawanga,
katika kumtafuta mtoto toka mafichoni kwa ajili ya kuokoa uhai wake. Jitihada zilizofanywa na jamii ya
Kapanga ni uthibitisho kuwa, ulinzi wa mtoto ni jukumu la wazazi, walezi na watu wote katika jamii.
Kwa niaba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, tunatoa pole kwa marafiki
wa mtoto, wazazi, ndugu na majirani na familia kwa ujumla, na tunawaomba kuwa na moyo wa subira
katika kipindi hiki cha majonzi makubwa.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
18/4/2016
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...