Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo la Dodoma , Beatus Kinyaiya katika mazishi ya Askofu Mstaafu wa Dodoma Mathias Isuja yaliyofanyika kwenye kanisa kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba Mjini Dodoma Aprili 20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mathias Isuja katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba Aprili 20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mathias Isuja katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba, Aprili 20, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya waumini na wakazi wa mkoa wa Dodoma
katika mazishi ya Mhashamu Askofu Mstaafu, Mathias Isuja wa Kanisa Katoliki
Jimbo Kuu la Dodoma.
Amesema
kifo hicho ni pigo kwa watu wote na si kwa kanisa pekee kwa sababu walimtegemea
kulisaidia Taifa kiroho na kimaendeleo.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 20, 2016) wakati akizungumza na
waumini na wakazi wa mkoa huo na mikoa jirani kwenye ibada ya mazishi
iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiaskofu la Mtume Paulo wa Msalaba mjini Dodoma.
Askofu
Isuja ambaye alizaliwa Agosti 14, 1929 alikuwa Askofu wa kwanza mzalendo katika
Jimbo la Kanisa Katoliki la Dodoma. Alistaafu kazi ya uaskofu mwaka 2004 kwa
mujibu wa sheria ya kanisa. Alifariki Aprili 13, mwaka huu.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kumuenzi Askofu Isuja kwa kazi nzuri
aliyoifanya wakati wa uhai wake na kuyaendeleza yote aliyoyaanzisha kwenye
maeneo aliyowahi kuyatumikia.
“Tumepoteza
mtu makini, sisi ni mashahidi wa mchango mkubwa wa marehemu siyo tu katika
kutoa huduma za kiroho, bali pia huduma za kijamii zilizolenga kuleta maendeleo
kwa wananchi katika jimbo hili la Dodoma na katika taifa kwa ujumla,” amesema.
Mapema, akitoa
mahubiri wakati wa ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu
Judathadeus Ruwa’ichi alisema waumini wa kanisa hilo wa mkoa wa Dodoma na Tanzania
nzima wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha marefu aliyomjalia Askofu
Isuja.
“Tunapaswa
kumshukuru kwa maisha marefu ambayo Mungu alimzawadia baba yetu Isuja. Katika
Zaburi ya 90 tunasoma kuwa mwanadamu ana miaka ya matazamio ambayo ni 70,
lakini yeye alipewa miaka ya matazamio 70 na akazawadiwa nyongeza ya miaka 10
na kisha miaka mingine sita na nusu,” alisema.
Alisema
zawadi nyigine ambayo Mungu aliwapatia waumini hao ni ya imani ambayo Baba
Askofu Isuja aliipokea, aliifundisha na aliishi na akawataka waendelee
kumshukuru Mungu kwa hilo. “Miaka 56 ya utumishi wake kama padre na askofu ni
zawadi kwa Dodoma na Tanzania na siyo kwake yeye binafsi,” alisema.
Ibada hiyo
ya mazishi ilihudhuriwa na Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa kawaida 28 kutoka
majimbo ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Njombe, Mpanda, Iringa, Songea, Tabora,
Morogoro na Mahenge. Mengine ni Musoma, Rulenge, Mbinga, Moshi, Same, Kahama,
Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara na Lindi. Majimbo mengine ni Bukoba, Tanga,
Singida, Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Kondoa na Kayanga.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L.
P. 980.
DODOMA.
JUMATANO,
APRILI 20, 2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...