Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
KIKOSI cha Mbeya City Fc kesho jumapili kinashuka kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika mchezo wa kufungia msimu wa 2015/16 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya wageni wao Ndanda Fc 'wana kuchele' kutoka mkoani Mtwara.
Meneja wa kikosi cha City, Geoffrey Katepa amesema kuwa nyota wote 18 wametayarishwa kwa ajili ya kuwakilisha timu yao na wako kwenye hali nzuri na tayari kabisa kusaka ushindi.
“Kama unavyoona tumemaliza mazoezi muda huu, yalikuwa ni mazoezi mepesi kuelekea mchezo wa kesho kila mmoja yuko vizuri na ana ari kubwa, jambo muhimu kwetu ni kushinda mchezo huo ili tumalize ligi kwa heshima, hatuna wasiwasi wowote tuko salama kwenye msimamo wa ligi, kumaliza kwa ushindi kutatuweka kwenye mapumziko mazuri kwa matayarisho ya msimu mpya”, amesema Katepa.
Kuhusu majeruhi Katepa alisema kuwa City itakosa huduma ya nahodha na mlinzi shupavu wa kushoto Hassan Mwasapili aliye majeruhi kufuatia maumivu ya nyama za paja yanayomkabili, pia Temi Felix na Deo Julius hawatakuwa sehemu ya mchezo wa kesho kupisha majeraha waliyonayo.
“Mkuu wa kitengo chetu cha utabibu Dr Joshua kaseko, amenieleza asubuhi kuwa tutawakosa wachezaji hao kutokana na majereha waliyonayo hii ina maana kuwa wataonekana uwanjani wakati wa matayarisho ya msimu mpya, mwalimu tayari kashafanya utaratibu wa wale wataochukua nafasi zao hivyo tuna uhakika wa kuingia uwanjani na kikosi kilicho bora licha ya kuwakosa hao tutahakikisha ushindi unapatikana.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...