Meya wa Jiji la Dare s Salaam Mh. Issaya Mwita
ameipongeza klabu ya Yanga kwa kunyakua ubingwa huo kwa mara ya Ishirini na
Sita tangu kuanzishwa kwa mashindano ya ligi kuu hapa nchini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mh. Mwita
amesema ushindi wa Klabu ya Yanga umeliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuendelea
kupata sifa katika medani ya Kitaifa na Kimataifa kutokana na ushiriki wa klabu
hiyo katika mashindano ya kimataifa.
“Ninaiomba klabu ya Yanga kuthamini ubingwa wao kwa
kuonyesha viwango vya kimataifa ili kulifanya jiji hili kuwa chuo cha mafunzo
ya mchezo wa mpira wa miguu,” alisema Mh. Mwita.
Aidha aliliomba Shirikisho la Mchezo wa MPira wa
Miguu nchini (TFF) kuendelea kusimamia ligi kwa ustadi zaidi ili kulingana na taratibu za mpira wa
miguu kama zinavyoainishwa na Shirikisho la
Soka duniani (FIFA) pamoja na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).
“Naomba nitoe wito kwa wadau wote katika familia ya
mpira wa miguu kushirikiana ipasavyo ili kufanya ligi yetu iwe miongoni mwa
ligi bora barani afrika na Duniani kwa ujumla,” aliongeza Mh. Mwita.
Pia aliwapongeza wadhamini wote waliojitolea
kusaidia ufadhili kwa vilabu vyote vilivyoshiriki ligi kuu na kuwataka
waendelee kuwasaidia ili kuinua soka letu la bongo.
Aidha ameitakia klabu ya Yanga ya Jangwani
maandalizi mema katika mchezo wa marudiano wa kufuzu hatua za makundi ya kombe la Shirikisho la mpira wa
miguu Barani Afrika (CAF) dhidi ya klabu ya Sagrada Esperance huko nchini
Angola.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...