Na Mwandishi Maalum.
Umoja wa Mataifa umeipongeza Tanzania kwa namna
ambavyo imechukua hatua za haraka za kukabiliana na tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia zinazowahusisha
baadhi ya walinzi wa amani wanaohudumu katika Misheni ya Kulinda Amani
katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(
DRC)
“Tanzania imeweza ndani ya siku tano tangu kupokea tuhuma dhidi
ya walinzi wake wa amani kuunda timu
ya kitaifa ya uchunguzi kwajili ya kuzifanyika kazi tuhuma hizo. Hatua hii na utashi ulioonyeshwa na Tanzania
ni hatua nzuri na inayopashwa kupongezwa na inaonyesha namna gani inavyochukulia
kwa uzito wa hali juu tuhuma hizo”.
Pongezi hizo zimetolewa
mwishoni wa wiki ( Ijumaa) na Bw. Atul Khare, Naibu Katibu Mkuu Mwandamizi anayeongoza Idara ya Field Support katika Umoja wa Mataifa.Mwishoni mwa wiki ,
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,
aliandaa mkutano ambao ulikuwa na
lengo la kutoa taarifa ya maendeleo
na mwelekeo wa Umoja wa Mataifa katika
kukabiliana na tuhuma za udhalilishaji
wa kijinsia zinazowakabili walinzi wa
Amani wa Umoja wa Mataifa, walinzi wa
Amani wa Kimataifa, na wafanyakazi raia.
Katika taarifa yake,Bw. Khare amesema, utaratibu uliopo
unaitaka nchi ambayo walinzi wake wametuhumiwa kujihusisha na vitendo vya
udhalilishaji pamoja na hatua nyingine,
kuunda timu yake ya kitaifa ya uchunguzi
ndani ya siku kumi, lakini Tanzania
iliunda timu hiyo ndani ya siku
tano na kuanza kazi jambo ambalo
amesisitiza linapashwa kuigwa na nchi nyingine.Akabainisha kwamba
kinachosubiriwa sasa kutoka Tanzania
ni taarifa rasmi ya kukamilishwa kwa
uchunguzi huo na hatua ambazo zitakuwa zimechukuliwa kwa walinzi ambao watakuwa
wamethibitika kujihusisha na vitendo hivyo.
Tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia
dhidi ya baadhi ya walinzi hao wa
Amani wa Tanzania ziliibuliwa na Umoja
wa Mataifa mwezi March mwaka huu.Akizungumza katika mkutano huo,
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, amesema utovu wa nidhamu uliofanywa na walinzi wachache hauwezi
kuchafua kazi nzuri na sifa ya kutukuka ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika
Misheni mbalimbali za kulinda Amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Akasema Balozi, ni kwa kutambua kazi hiyo ya kutukuka na ambayo pia imepelekea baadhi ya wanajeshi wa Tanzania kupoteza
maisha yao kishujaa wakati wakiwasaidia wananchi wa mataifa mengine kuwa na amani.
Tanzania inalichukulia kwa uzito wa kipekee
tuhuma za udhalilishaji wa
kijinsia na kwamba wale wote wataokabainika hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za
nchi.
Akaongeza kwamba Tanzania imeamua kuwaalika wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa kwenda nchini
Tanzania ambapo watashirikiana na
wakufunzi wa JWTZ katika kuimarisha mitaala ya ufundishaji inayohusiana na masuala ya ulinzi wa raia hususani eneo la
udhalilishaji wa kijinsia.
Vilevile Balozi Manongi amesema
Tanzania itaendelea kushirikiana na
Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba vitendo hivyo viovu dhidi ya raia wasiokuwa na hatia vinakomeshwa
ili pamoja na mambo mengine kurejesha
heshima ya Umoja wa Mataifa na heshima
ya nchi zinachochangia wanajeshi na polisi katika misheni za kulinda Amani.
Lakini kubwa zaidi kurejesha imani kwa
wananchi wanaohitaji ulinzi.
Akielezea kwa ujumla kuhusu
kadhia hiyo ya udhalilishaji wa kijinsi, Bw. Khare amesema, nchi nyingine zinazochangia walinzi wa Amani na ambazo pia walinzi wao wametuhumiwa zinaendelea
ushirikiano kwa kuchukua hatua
mbalimbali ingawa pia zipo zinazosuasua.
Nchi ambazo zimetoa ushirikiano ukiacha
Tanzania ni Afrika ya Kusini, DRC, Misri na Bangladesh
Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwafikisha katika mahakama za kijeshi wale
wanaokutwa na hatia, kufungwa, kufukuzwa
kazi na kutoshiriki kabisa katika misheni za
kulinda Amani na kutoa misaada kwa
wahanga.
Akaongeza pia kwamba nchi nyingi zimeimarisha mitaala ya ufundishaji kwa
walinzi wa amani, kuandaa timu za
uchunguzi ambazo zinakuwa tayari wakati wowote zitakapohitajika, huku nyingine zikihakikisha kwamba zinakuwa na
wataalamu wa masuala
ya sheria miongoni mwa walinzi wa
Amani.
Bw. Khare amesisitiza Umoja wa
Mataifa unatambua mchango mkubwa wa walinzi wa Amani pamoja na mazingira magumu
ya utekelezaji wa mamlaka yao. Hata
hivyo anasema vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia havipashwi kuvumiliwa wala
kufumbiwa macho na kwamba kila nchi
inaowajibu wa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria watuhumiwa wanaothibitika kuhusika na
ukatili huo na kwamba ushirikiano
na misaada kwa waathirika ni jambo la
muhimu sana.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako
Manongi akizungumza wakati wa mkutano wa kupokea taarifa kuhusu
jitihada zinazofanywa na Umoja wa Mataifa za kukabiliana na tuhuma za
udhalilishaji wa kijinsia katika misheni za kulinda amani. Katika
mchango wake Balozi amesema Tanzania haitawavumilia walinzi wa amani
wachache ambao wanaharibu kazi nzuri na sifa ya kutukuka ya JWTZ
katika Misheni za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa. Na kwamba wale
watakaothibitishwa kujihusisha na tuhuma hizo watachukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria za nchi.

Naibu Katibu Mkuu Mwandamizi, Bw. Atul Khare akitoa taarifa kuhusu
mwelekeo na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia. katika taarifa yake ameipongeza Tanzania
kwa namna ambayo iliitikia kwa haraka wito wa kuunda timu ya kitaifa ya
uchunguzi ndani ya siku tano badala ya siku kumi kama taratibu
zinavyoainisha na kwamba hatua hiyo ya Tanzania inapashwa kuigwa na
nchi nyingine.



Hata huko Bungeni wabunge wanawake wamedai kudhalilishwa. Kama Taifa tuhakikishe tunayakomesha yote haya popote pale. Tusikubali kuharibu heshima ya JWTZ ama chombo chochote. Tukomeshe kweli isiwe maneno tu ya Mabalozi.
ReplyDelete