Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
KATIBU mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohammed Kiganja amewataka walimu wa shule za msingi nchini, wanaoandaa timu kwa ajili ya mashindano ya Umitashumta kuepuka kuwatumia wachezaji mamluki katika mashindano hayo ambayo yanaendelea nchi nzima katika ngazi mbalimbali.
Kiganja amesema hayo juzi alipoitembelea kambi ya mazoezi ya timu ya Umitashumta ya Manispaa ya Kinondoni katika shule ya Sekondari ya Lord Baden iliyoko Bagamoyo mkoani Pwani na kwa kuwatumia mamluki katika mashindano hayo ni kuyaondolea hadhi na kuwanyima haki walengwa hali ambayo alisema ni makosa kisheria na kwamba, yeyote atakaethubutu kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
"Mashindano haya ni kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi, naomba washirikishwe hao tu, kamwe msijaribu wala kuthubutu kuwatumia mamluki katika mashindano hayo, sioni mantiki ya kufanya hivyo, waandaeni wanafunzi wenu kwa ushindani itakuwa vizuri kuliko kutumia mamluki ili kupata ushindi wa hila, akibainika mwalimu ametumia mamluki katika timu yake, ngazi husika za maamzi zimchukulie hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na timu yake kufutwa na kuondolewa mashindano" amesema Kiganja.
Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni Kiduma Mageni mbali na kumshukuru Kiganja alimhakikishia kuwa, timu yake haitakuwa na mchezaji mamluki hata mmoja, haijawahi na haitatokea na kuunga mkono kuchukua hatua dhidi ya watakaobainika kuwatumia wachezaji mamluki.
Naye mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano Umitashumta Manispaa ya Kinondoni, Masau Bwire amesema katika mashindano ya Mkoa wa Dar es salaam yanayoanza Ijumaa hii Juni 10, 2016 katika viwanja vya Chuo Kikuu, Mlimani yakishirikisha timu za Manispaa ya Kinondoni, Ilala na Temeke hawatarajii kuwepo kwa vitendo vya kihuni kwa timu kuchezesha wachezaji mamluki na ikitokea, walimu waliohusika ni majipu tayari, lazima watumbuliwe!
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...