Wakati Marekani ikiadhimisha miaka 240 ya Uhuru wetu, ninakumbushwa kwamba nchi yetu,
kama ilivyo kwa Tanzania, imedhamiria kuimarisha amani, utulivu, na ukuaji wa uchumi kwa
raia wake wote. Tarehe 4 Julai, tunasherehekea Katiba yetu tunayoienzi, ambayo ni nyaraka
inayotupa na kutuhakikishia haki binafsi kama vile uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na
uhuru wa vyombo vya habari. Tuna fahari kwa demokrasia yetu ya uwakilishi ambayo kwa
karne kadhaa imewezesha kuwekwa kwa mifumo ya kuhakikisha uwiano wa mamlaka baina ya
mihimili ya utawala (checks and balances) katika kulinda amani na ustawi wa raia wetu wote.
Hivi sasa kampeni kali za uchaguzi wa Rais ajaye wa Marekani zinaendelea. Rais ajaye wa
Marekani atakuwa na nguvu kubwa katika kuweka sera, lakini atakuwa akifanya kazi katika
mfumo wenye nyenzo za kuwianisha mamlaka kama ilivyoelezwa hapo juu. Nyenzo hizo ni
pamoja na mahakama imara, mhimili wa bunge lenye sehemu mbili na vyombo huru vya habari
vinavyowapa Wamarekani, taarifa, maoni na mawazo mbalimbali.
Kwa hali hiyo, ninaguswa
pale sauti za Kitanzania zinapopazwa na kutoa malalamiko kuhusu kuminywa kwa demokrasia,
iwe ni kwa kupiga marufuku mikutano ya kisiasa au kuzuia matangazo ya televisheni ya vikao
vya Bunge. Ninaamini kwamba mapambano dhidi ya rushwa – ambayo kwa hakika ni muhimu
sana kwa nchi zetu mbili – ni lazima yafanyike bila kukwaza majadiliano, hali ya kutofautiana
maoni au kuwepo kwa uhuru wa kujieleza. Ukweli ni kwamba mkinzano wa kibunifu kati ya
mawazo tofauti yanayoshindana ndiyo huifanya demokrasia kuimarika, kustawi na kuwa hasa ya
uwakilishi wa watu.
Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wangu, ninaunga mkono azma ya Tanzania ya kudumisha na
kuimarisha amani na ustawi. Kwa hakika watu wa Marekani tunajivunia urafiki wetu wa muda
mrefu na watu wa Tanzania. Aidha, tuna fahari kuwa mbia mkubwa zaidi wa maendeleo nchini
Tanzania na kuendelea na uwekezaji wetu katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na afya, elimu,
kilimo na ukuaji wa uchumi.
Malengo yetu ya pamoja na urafiki wetu unadhihirishwa na
kufanana kwa mijadala ya umma katika nchi zetu kuhusu mifumo ya kuwianisha mamlaka
miongoni mwa mihimili ya serikali na umuhimu wa kuwa na vyombo huru vya habari
vinavyoweza kuripoti kwa usahihi utendaji wa serikali kwa raia.
Majadiliano ya wazi kuhusu
uwezo wa serikali kuwasilisha kwa uaminifu matakwa ya raia wake na kulinda amani na ustawi
ndiyo yaliyoiwezesha nchi yangu kujitangazia uhuru wake miaka 240 iliyopita. Wamarekani
walijitahidi sana wakati huo, na tunaendelea kujitahidi hivi leo kupitia majadiliano haya makali
katika jamii na siasa. Ninaamini kwamba Marekani, na nchi zote zenye demokrasia yenye afya
zinaimarika zaidi na zaidi kutokana na majadiliano haya.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...