Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imewatahadharisha wananchi wanaopanga kusafiri kwenda nje ya nchi
kuhakikisha kuwa wanafika katika vituo vya afya na kuchanjwa chanjo ya
kuzuia maambukizi ya Homa ya Manjano badala ya kuwalipa fedha baadhi ya
watumishi wa afya wasio waaminifu ili watengenezewe kadi hizo kinyume
cha sheria.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema
Rusimabayila akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo leo jijini Dar es
salaam amesema baadhi ya wasafiri wamekuwa wakishirikiana na watumishi
wa afya wasiowaaminifu kwa kuwalipa fedha ili waweze kuwatengenezea
kadi hizo na kisha kuzitumia nje ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa
usalama wa Afya zao.
“Kumekuwa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu ambao
hupokea fedha na kisha kutengenezesha kadi za wasafiri zinazoonesha
kuwa wamepatiwa chanjo, Jambo hili ni hatari kwa afya ya msafiri, sasa
tunaona mlipuko wa ugonjwa huu ukitokea katika nchi za karibu ni muhimu
mtu kuchanja ili kuepuka kuwa chanzo cha kuleta ugonjwa huu” Amesisitiza
Dk.Neema.
Amesema ni jambo lisilokubalika kwa msafiri kuwa na
kadi ya chanjo ya Kinga ya Homa ya Manjano akijua kabisa hajapatiwa
chanjo hiyo na kuongeza kuwa jambo hilo linamuweka muhusika katika
hatari ya kupata maambukizi akisafiri kwenye nchi zenye mlipuko wa
ugonjwa huo.
“Napenda kusisitiza kuwa ni muhimu sana msafiri
akachanjwa chanjo hii kwa ajili ya kinga ya afya yake mwenyewe, kupata
kadi bila kuchanjwa na kwenda mahali ambapo kuna ugonjwa huu ni
kujidanganya, epuka kuwa chanzo cha kusambaza ugonjwa huu” Amesisitiza
Dk. Neema.
Kuhusu gharama za chanjo hiyo amesema kuwa msafiri
anayetaka kupata chanjo hiyo anatakiwa kulipia gharama ya Elfu Ishirini
(20,000/=) ikiwa ni malipo halali ya Serikali na mlipaji hupatiwa
stakabadhi halali.
Aidha, amesema mbali na hatua zinazochukuliwa
kudhibiti hali hiyo, Wizara inakamilisha utaratibu wa kuwa na kadi
maalum ambazo zitakuwa tofauti, zenye nembo maalum ambazo mtu hataweza
kughushi wala kufanya udanganyifu wa aina yoyote.
Mkurugenzi
wa Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa
ufafanuzi kuhusu Chanjo ya Homa ya Manjano na vitendo vya baadhi ya
watumishi wa afya wasiowaaminifu ambao hulipwa fedha ili waweze
kuwatengenezea wasafiri kadi za Chanjo ya Homa ya Manjano na kisha
kuzitumia nje ya nchi jambo ambalo kinyume cha sheria na hatari kwa
usalama wa Afya zao. Picha/Habari na Aron Msigwa – MAELEZO.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...