WAJASIRIAMALI nchini wameshauriwa
kujitokeza kwa wingi kwenye maonyesho mbalimbali yanayoandaliwa na Shirika la
kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO),ili kuweza kuzitangaza bidhaa zao na kujifunza
mbinu za kuboresha thamani bidhaa wanazozitengeneza.
Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi
Profesa Sylvester Mpanduji, amesema maonyesho ya biashara kwa wajasiriamali
yana umuhimu mkubwa kwani hutoa fursa ya kipekee kwa kujifunza na pia kutafuta
masoko ya bidhaa.
“Maonyesho ya kikanda yanayoandaliwa na SIDO yanawaleta
pamoja wajasiriamali wengi wakiwepo wale wanaotoka nchi za jirani ambao nao
huja na bidhaa mbalimbali kuzionyesha na kuzinadi kwenye maonyesho,” Profesa
Mpanduji alisema.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu maonyesho ya Kanda ya Kusini ambayo
yanatarajiwa kufunguliwa kesho jijini Mbeya na kumalizika Oktoba 4, Profesa
Mpanduji amewaka wajasiriamali kuchangamkia fursa za maonyesho hayo kuzitangaza
bidhaa zao.
“Zaidi ya wafanyabiashara zaidi
ya 200 wamethibitisha kushiriki kwenye maonyesho hayo,” alisema na kuongeza
kuwa SIDO kwa kushirikiana na wadau wengine imejidhatiti kuhakikisha kuwa
bidhaa zinazotengeneza na wajasiriamali wadogo zinakuwa na ubora unaostahili na
kushindana kimataifa.
Profesa Mpanduja alisema bidhaa
mbalimbali za ngozi, kusindika na mikono zitakuwepo kwenye maonyesho na pia
wajasiriamali kutoka nchini Kenya watashiriki.
“Haya ni maonyesho ya 98 na SIDO
inayapatia kipaumbele kikubwa kwani yanatoa fursa kwa wajasirialimali kujifunza
mbinu na maarifa yakufanya biashara ikiwemo kupata masoko, mikopo na pia namna
ya kuboresha bidhaa zao,” alisisitiza.
Alizitaja baadhi ya Taasisi za
fedha kama benki za CRDB, NMB, Diamond
Trust kuwa nazo zitashiriki kwenye maonyesho hayo ya kanda ya kusini ambayo
inaundwa na mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Iringa na Njombe.
“Shirika la Viwango nchini (TBS),
Mamlaka ya Dawa na Chakula (TDFA) pamoja na Mamlaka ya Biashara nchi
(TAN-TRADE) watashiriki katika maonyesho hayo muhimu,” Profesa Mpanduji
alisema.
Profesa Mpanduji ametoa wito kwa
wajasiriamali kutoka katika kanda
nyingine za jirani kujitokeza na kuchangamkia fursa za maonyesho hayo ya
kipekee.
“Ninapenda kupongeza mwamko
mkubwa wa wajasiriamali na wanavyotengeneza bidhaa za kiwango cha juu,” alisema
na kuongeza kuwa wakati umefika kwa watanzania kununua na kujivunia bidhaa
zinazotengenezwa hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi
Profesa Sylvester Mpanduji, akisisitiza jambo wakati akiongea na waandishi wa
habari, jijini Dar es Salaam jana kuhusu maonesho ya wajasiriamali kwa kanda ya
kusini yanayoanza Mkoani Mbeya kesho ambapo washiriki zaidi ya 200
wamethibitisha ushiriki wao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...