Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kujipanga na kuanza mkakati wa kutangaza
huduma za fedha ambazo zitatolewa na kampuni hiyo mwanzoni mwa mwaka ujao.
Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo baada ya kukagua mitambo itakayotumika kwa
huduma hiyo ambayo itaongeza ushindani wa biashara kwenye huduma za simu nchini
mkoani Dodoma.
"Lazima mjipange kwenye idara ya masoko kwa kuanza kutangaza huduma hiyo kupitia
njia zote zikiwemo mitandao ya kijamii, ili wananchi warahisishiwe huduma za fedha
kupitia TTCL", amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha, ameiagiza kampuni hiyo kupitia idara ya masoko kujipanga kuona fursa zilizopo
kwa kufahamu mahitaji ya wateja wao na kuhakikisha inaongeza wateja katika mkoa
huo ili kuteka soko la ushindani ambapo Serikali inajipanga kuhamia huko.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya watendaji wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), alipokuwa akikagua mitambo ya kutolea huduma za kifedha iliyopo katika ofisi za Kampuni hiyo mkoani Dodoma.
Waziri Prof.Mbarawa ametaja baadhi ya maeneo ambayo TTCL inahitaji kuboresha
zaidi ni upande wa Simu (Voice) na Data (video) ili kuweza kurahisisha mawasiliano
kwa njia ya video conference kwa kuwa kuna baadhi ya watendaji wengine watabaki
Dar es salaam.
"Mkiimarisha mawasiliano upande wa data mtarahisisha hata maamuzi na pia kazi
zitaenda vizuri Serikalini hasa ukizingatia baadhi ya watumishi watakuwa hapa Dodoma
na wengine Dar es Salaam", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Sambamba na hilo, Waziri Mbarawa ameliagiza Shirika la Posta nchini kuja na mkakati
wa kuandaa matangazo ya kutambulisha huduma ya Posta mlangoni kwa jamii ili
kuiwezesha huduma hiyo kutambulika kirahisi.
Mhandisi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Paul Magembe akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, kuhusu mitambo ya kutolea huduma za kifedha iliyopo katika ofisi za Kampuni hiyo mkoani Dodoma.
Amesisitiza kwa Taasisi hizo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kufikia malengo
waliojiwekea na kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Akiwa mkoani humo Prof. Mbarawa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa, Jordan
Rugimbana kuboresha miundombinu nchini hususan katika mkoa huo ikiwemo
kuboresha usafiri wa anga katika uwanja wa ndege wa Dodoma ili kuruhusu ndege
kubwa kuweza kuruka na kutua.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ameongea na watendaji pamoja na wafanyakazi
wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake na kusisitiza kufanya kazi kwa kasi, uadilifu,
ubunifu na kushirikiana katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi hao Meneja wa Wakala wa Majengo(TBA)
mkoani humo, Arch. Masalu Bururu, amemuahidi Waziri huyo kutekeleza yale yote
aliyowà agiza ili kuleta ufanisi na tija kwa Taifa.
Waziri Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku kumi katika mikoa ya Mwanza,
Mara, Arusha, Manyara na Dodoma ambapo ametembelea miradi mbalimbali ambayo
inatekelezwa na Wizara hiyo.
Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), Mkoa wa Dodoma, Eng.
Bikulamchi Liberatus, akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof.
Makame Mbarawa, kuhusu mikakati ya utengenezaji wa magari katika karakana iliyopo Mkoani
humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...