Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) limeanza zoezi maalum la kuondoa mita za
Maji zote chakavu na za muda mrefu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam pamoja na miji ya
Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani ili kuweza kuongeza ufanisi katika usomaji wa Mita, kupunguza kiasi
cha Maji kinachopotea na kutoa matumizi halisi ya Maji yanayotumiwa na mteja.
Akizungumzia wakati wa zoezi hilo hilo, Kaimu Meneja Uhusiano wa Dawasco, Bi. Everlasting Lyaro
ameeleza kuwa shirika linaendelea na zoezi la kubadilisha mita za Maji zote ambazo ni mbovu na zenye
umri mkubwa kwenye maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na maeneo ya mkoa wa pwani
ambapo mita takribani 25,000 zimekwisha badilishwa hadi kufikia sasa.
“Shirika linaendelea na zoezi la kuondoa mita za Maji ambazo ni chakavu na za muda mrefu, tayari
tumefanikiwa kubadilisha Mita mpya za Maji zipatazo 25,000 katika makazi ya watu, taasisi pamoja na
viwanda na lengo letu mi kuweza kubadilisha Mita za Maji zipatazo 85,000 hadi kufikia mwisho wa mwaka
huu ili kusaidia kutoa matumizi halisi ya Maji yanayotumiwa na mteja wetu” alisema.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa wafanyakazi wanaofanya zoezi hilo na
endapo watapata wasiwasi basi waulize vitambulisho vya kazi ili kuepuka utapeli.
“Wananchi watupe ushirikiano ili zoezi hili lifanikiwe na kukamilika kwa wakati kwani lina faida kwetu sisi
kama shirika na kwa mteja. Pia tukumbuke kuwa zoezi hili ni bure hivyo wananchi wasidanganywe
kuchangia hela yoyote” alimalizia Bi Lyaro
Wakizungumzia juu ya zoezi hili wananchi wanaohudumiwa na shirika hilo akiwemo Bi. Hadija Omary
mkazi wa Mwananyamala A, amepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Dawasco kwani itasaidia kuondoa
kero iliyokuwepo ya mita hizo kuvuja na kupelekea bili Maji ya mteja kuwa kubwa.
“Tumefarijika sana kuona Dawasco wameanza kubadilisha mita zao kwani ni za muda mrefu na zimekuwa
zikivujisha Maji na kupelekea bili zetu za maji kupanda kila wakati” alisema.
Naye, Bw. Boniface Mwakipesile, mkazi wa Mikocheni B, amezilalamikia mita hizo mpya na kudai kuwa
tangu zilipofungwa bili yake ya Maji imepanda ikilinganishwa na siku za nyuma, hivyo ameshauri elimu
zaidi itolewe kuhusiana na mita hizo.
“Mita hizi mpya za Maji mimi binafsi sizielewi kabisa, tangu zilipofungwa nashangaa bili yangu ya Maji
inakuja tofauti, imekuwa kubwa sana ikilinganishwa na zamani hivyo Dawasco wazidi kutuelimisha zaidi
maana wengi wanaziona kama mita za mwendo kasi” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...