Katika kuitikia wito wa serikali ya Awamu ya Tano wa Kujenga Tanzania ya Viwanda, Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Magereza (Corporation Sole) limeingia ubia na Mifuko ya Jamii ya PPF na NSSF wa kufufua kilichokuwa kiwanda cha Sukari kilichopo Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro.
Kiwanda cha sukari cha Mbigiri kilisimamisha uzalishaji tangu mwaka 1996 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa mitambo. Lakini kutokana na kuwa eneo zuri kimkakati yaani uwepo wa raslimali ardhi ya kutosha, nguvu kazi ya baadhi ya wataalam wa zamani wa kiwanda hicho, chanzo cha maji kuwezesha kuendesha kilimo cha umwagiliaji kumezishawishi taasisi zingine kushirikiana na Jeshi la Magereza kuwekeza katika eneo hili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kukagua eneo la Uwekezaji, Kaimu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma Malewa amesema uwekezaji huu utakuwa na faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira, upatikanaji wa sukari ya kutosha nchini lakini pia wakulima wa eneo hilo watapata soko la uhakika la kuuza miwa katika kiwanda hicho.
Aidha Kaimu Kamishna huyo ametoa wito kwa wananchi kutovamiwa maeneo ya majeshi kwani mengi yamehifadhiwa kwa shughuli za baadae zenye maslahi mapana kwa taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPF William Erio amesema matarajio yao ni kuona kiwanda kinaanza mapema iwezekanavyo hivyo, ametoa wito kwa wananchi wa maeneo jirani kuchangamkia fursa ya kulima zao la miwa kwa maana sasa watakuwa na uhakika wa soko lililo karibu nao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kyaharara amesema kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 30,000 kwa mwaka na kitahitaji tani 500,000 za miwa hivyo ni fursa nzuri kwa wananchi wa maeneo jirani.
“Ni matarajio yetu kuwa kiwanda hiki kitaongeza ajira, kitainua uchumi kwa wafanyakazi na wanakijiji, tutapata wanachama wengi zaidi lakini pia tutakuwa tumeongeza uwezo wetu vizuri zaidi wa kuwahudumia wanachama wetu kupitia uwekezaji huu” Alihitimisha Prof. Kahyarara.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa (mwenye miwani) na ujumbe wake wakiwasili Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro jana tarehe 26.01.2017 tayari kwa kukagua eneo la uwekezaji wa Kilimo cha Miwa na Uzalishaji wa Sukari. Wa kwanza nyuma yake ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof.Godius Kahyarara, mshauri mwelekezi katika mradi huo ndugu Seleman Karanga akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa PPF ndugu William Erio.
Ujumbe wa Uwekezaji wa Ubia katika kiwanda cha sukari cha Mbigiri kati ya Mifuko ya Jamii ya NSSF, PPF na Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Magereza (Corporation Sole) wakikagua baadhi ya maeneo ya ndani ya kiwanda cha zamani cha sukari cha Gereza hilo kilichosimamisha uzalisha zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Ujumbe wa Uwekezaji wa Ubia katika kiwanda cha sukari cha Mbigiri kati ya Mifuko ya Jamii ya NSSF, PPF na Jeshi la Magereza wakipata maelezo kutoka kwa Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Angolwise Pilla (wa pili kushoto) ambaye ni mfanyakazi wa zamani kilichokuwa kiwanda cha sukari cha Gereza Mbigiri kilicho simamisha uzalisha zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Viongozi waandamizi kutoka Jeshi la Magereza, PPF na NSSF wakipata maelezo ya namna kiwanda cha sukari cha Gereza Mbigiri mkoani Morogoro kilivyokuwa kikifanya kazi kutoka kwa mfanyakazi wa zamani wa kiwanda hicho Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Angolwise Pilla (wa nne kushoto). Viongonzi hao walitembelea kiwanda hicho jana ikiwa ni hatua za awali za uwekezaji wa ubia katika uzalishaji wa sukari nchini kati ya Taasisi hizo tatu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...