Na Humphrey Shao, Globu ya jamii
KIPA wa Kagera Sugar, David Burhan amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Bugando Jijini Mwanza, baada ya kuugua ghafla.
Kocha wa timu ya Kagera Sugar, Mecky Mexime, amethibitisha kutokea kwa kifo cha mchezaji wake huyo na kusema kuwa, Burhan alikuwa anasumbuliwa na Malaria.
Aidha Mexime amesema kuwa matatizo hayo yalianza wakati wamekwenda Singida kucheza na wenyeji wao, Singida United mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania, maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) katikati ya wiki.
Amesema alipanga kumuanzisha David Burhan katika mchezo huo, lakini hali yake ikabadilika ghafla hivyo akampanga kipa mwingine, Juma Kaseja badala yake.
“Tumecheza mechi, baada ya mechi wakati tunarudi, tunafika Biharamulo, macho yake yakaanza kubadilika yakawa ya njano, ikabidi alazwe pale, kesho yake akahamishiwa hospitali ya mkoa wa Kagera, ambako baada ya kupimwa wakasema apelekwe Bugando,”amesema Mexime.
“ uongozi wa Kagera Sugar ukafanya jitihada za haraka kumchukulia ndege kwenda Bugando Mwanza ambako alifika jana na kuanza matibabu kabla ya kufariki dunia leo asubuhi” amesema Mexime.
Amesema Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kurejeshwa kwao Iringa na kuhusu mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Mexime amesema kwamba hawajajua kama utachezwa au la.
“Sasa hivi ndiyo tunakwenda kwenye kikao cha kabla ya mechi, Pree Match Meeting tukifika huko ndiyo tutajua, ila kwa kweli upande wetu wachezaji wote wameshitushwa mno na taarifa hizi na sidhani kama wapo tayari kwa mechi ya leo,”alisema.
Burham alijiunga na Kagera Sugar msimu huu akitokea Maji Maji ya Songea, ambayo nayo ilimtoa Mbeya City. Huyo ndiye aliyekuwa kipa wa kwanza Mbeya City wakati inapanda Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita chini ya kocha Juma Mwambusi na akawa kipa bora wa msimu wa 2013/2014.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...