Kaimu Kamishna wa Nishati na Madini, Ally Samaje (anayetoa maelezo) akielezea Mpango wa Serekali wakati wa kufunga Mgodi wa Buzwagi. Wengine katika picha ni Wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini na Viongozi Waandamizi kutoka Mgodi wa Buzwagi.
Na Rhoda James – Kahama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa ameuongoza ujumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Wizara ya Nishati na Madini ili kukagua na kuhoji utendaji na ushiriki wa mgodi wa Buzwagi katika masuala ya kijamii mkoani Shinyanga hivi karibuni.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeutaka Uongozi wa Mgodi wa Buzwagi kuwashirikisha wananchi pamoja na wafanyakazi wa Mgodi huo Mpango wa kuufunga Mgodi huo (Mining Closure plan) unaotarajia kufunga shughuli zake za uzalishaji wa Dhahabu ifikapo Desemba 2017, huku shughuli za uchejuaji zitaendelea kwa miaka miwili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Doto Mashaka Biteko (wa pili kushoto) akimsikiliza Meneja wa Mgodi wa Buzwagi, Assa Mwaipopo (hayupo pichani) akielezea shughuli za uzalishaji wa Dhahabu katika Mgodi huo. Kushoto kwake ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje na wengine ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Watumishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Wafanyakazi wa Mgodi wa Buzwagi.
Haja hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Doto Mashaka Biteko mara baada ya kuwasili na kukutana na uongozi wa mgodi huo wakati wa ziara hiyo ya ukaguzi wa mgodi huo.
Biteko alisema kuwa Wananchi na wafanyakazi lazima wawe sehemu ya ufungaji wa Mgodi huo kwa kuwa jambo hilo ni kubwa kwani litatikisa Uchumi wa wananchi wa Kahama na pia Halmashauri ya Kahama itakosa Ushuru wa Huduma ambazo Mgodi huo umekuwa ukilipa kila mwaka.
“Mgodi huo unalipa Ushuru wa Huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama na wafanyakazi katika mgodi huo wana ajira kwa hiyo mipango ya kufunga mgodi huo iwe sehemu ya wananchi kwa asilimia mia” alisisitiza Biteko.
Muonekano wa Mgodi wa Buzwagi katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Aidha Biteko alitaka ufafanuzi zaidi kutoka kwa Uongozi wa Mgodi huo ni sababu zipi zinazopelekea mgodi huo kufungwa. Vilevile, alitaka Uongozi kuijulisha kamati hiyo jambo ambalo mgodi huo unawaachia wanannchi wa Kahama mara baada ya shughuli za uzalishaji kufungwa.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...