Dodoma, Jumanne, Januari 31, 2017:  

Serikali leo imeainisha utekelezaji na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi katika sekta mbalimbali katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majibu ya Serikali kwa baadhi ya hoja ni kama ifuatavyo:

                          Ujenzi Nyumba za Walimu.

Akijibu hoja kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameliambia Bunge kuwa Serikali ilitenga kiasi cha Sh. Bilioni 13.9 katika Bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu wa Sekondari, na Shilingi bilioni 11.4 kwa nyumba za walimu wa Shule za Msingi.

Aidha, Waziri Jafo ameeleza kuwa tayari nyumba 146 za walimu zimeshajengwa nchini kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari. Pia amezungumzia Serikali kuanza kulipa madeni ya walimu.

                             Ujenzi wa Viwanda Nchini

Akijibu swali kuhusu uwekezaji wa viwanda nchini hususani mkoani Tabora ambako kuna kilimo cha Tumbaku na maeneo mengine yenye malighafi, Mhandisi Edwin Ngonyani kwa niaba ya Waziri wa Viwanda ameliambia Bunge kuwa tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Vietnam na kuzitaka Halmashauri zote nchini kuendelea kuitikia wito wa kutenga maeneo ya uwekezaji.

“Kituo cha uwekezaji Nchini (TIC) kimepewa maelekezo maalum kunadi fursa hii kwa wawekezaji katika sekta ya tumbaku na sigara hapa nchini,” alisema Mhandisi Ngonyani ambaye pia ni Naibu Waziri, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

                   Tupende Bidhaa Zetu.

Akijibu hoja kuhusu bidhaa nyingi za Kenya kuingia nchini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba amesema moja ya changamoto inazozikumba bidhaa za Tanzania ni wananchi wake kupenda vya nje.

“Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti na Kusimamia Uondoaji wa wa Vikwazo visivyo vya Kiforodha na kuhamasisha wafanyabiashara nchini kuzalisha bidhaa zenye ubora,” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...