JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA NISHATI NA MADINI
Wizara ya Nishati na
Madini inapenda kuufahamisha umma kuwa, zoezi
la kuwaokoa wachimbaji 15 waliofukiwa na kifusi
tarehe 26/01/2017 kwenye mgodi wa dhahabu eneo la kijiji cha Mawemeru,
Nyarugusu, Wilayani Geita limekamilika kwa mafanikio.
Ajali ya kufukiwa
wachimbaji hao iliyohusisha Watanzania 14 na raia mmoja wa China ilitokea kwenye
leseni ya uchimbaji wa Kati wa madini ya dhahabu yenye Namba ML 492/2013
inayomilikiwa na Bw. Ahmed Mubarak Adam. Chanzo cha ajali hiyo
ilikuwa ni kuanguka kwa shaft ya
mgodi huo na kufukiwa na kifusi wakati wachimbaji hao wakifanya kazi mgodini
chini ya ardhi.
Tukio la uokoaji
limefanikiwa leo tarehe 29/01/2017 ambapo wachimbaji hao walianza kutolewa shimoni
kuanzia saa 5 hadi saa 5:30 asubuhi wote 15 wakiwa hai ingawa walikuwa
wamedhoofika kiafya. Aidha, wachimbaji
hao wamepewa huduma ya kwanza katika eneo la ajali na kisha kukimbizwa
Hospitali Teule ya Rufaa ya Geita. Hadi sasa wachimbaji hao wapo Hospitali
wakiendelea na matibabu kwa uchunguzi zaidi wa afya zao.
Juhudi za kuokoa
wachimbaji hao ambazo zilifanyika kwa
kufukua kifusi katika eneo la ajali zilianza mara baada ya tukio hilo kutokea.
Uongozi wa Mkoa wa Geita ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Meja. Jen.(Mst) Ezekiel E.
Kyunga ulishirikiana na Wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni za
Madini mbalimbali mkoani Geita katika zoezi la ufukuaji kifusi ili kuokoa
maisha ya wchimbaji hao.
Kampuni zilizoshiriki
kwa kutoa mitambo na vifaa mbalimbali ni Kampuni ya Busolwa Mining Ltd; Kampuni ya Geita
Gold Mine (GGM); Kampuni ya Nyarugusu
Mining Ltd; Nsangano Mining Project; Metchell
Tanzania Drilling; WAJA Hospital pamoja
na wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Viongozi wa wachimbaji
madini Wilaya, Mkoa na Taifa.
Akizungumza mara
baada ya kuokolewa wachimbaji hao, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.
Medard amewashukuru wadau wote walioshiriki kwa hali na mali kufukua kifusi na
hatimaye kufanikiwa kuwatoa wachimbaji chini ya ardhi wakiwa hai.

Vilevile, amewataka
wachimbaji wawe watulivu katika kipindi ambacho tathmini ya hali ya usalama wa
mgodi inafanyika na kuagiza Uongozi wa Mkoa kuhakikisha kuwa ulinzi
unaimarishwa eneo la mgodi ili watu wasiweze kuingia na kuhatarisha maisha
yao.
Pia, ameagiza ukaguzi
wa kina ufanyike kwenye migodi mingine ya wachimbaji wadogo na ya kati eneo la
Nyarugusu na kwingineko nchini ili kuhakikisha kuwa migodi inakuwa salama kwa
wachimbaji wa migodi husika.
Imetolewa na;
KATIBU
MKUU
WIZARA
YA NISHATI NA MADINI
29/1/2017
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...