KASULU – Baadhi ya wakimbizi wanaoishi katika Kambi ya Nyarugusu, Magharibi mwa Tanzania wameanza kupokea fedha taslimu kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) katika hatua za awali za kubadilisha mfumo wa sasa wa kuwapatia chakula kila mwezi.
Wakimbizi wapatao 10,000 sasa wanapokea fedha taslimu kama sehemu ya mradi wa majaribio wa miezi mitatu. Mradi huu unafadhiliwa na nchi ya Canada kupitia mchango wake wa Dola za Canada 500,000 (Dola za Marekani 385,000) kwa WFP.
WFP itatoa Shilingi za Tanzania 10,000 (Dola za Marekani 4.50) mara mbili kwa mwezi kwa kila mwanakaya wa kaya iliyo katika mradi wa majaribio. Fedha itatumwa kwa mlengwa kupitia mtandao wa simu. Katika kipindi chote cha mradi, wakimbizi wataendelea kupata mgao wa mafuta ya kupikia yalioongezewa virutubisho na mchanganyiko maalumu wa uji wakati ambapo badala ya mahindi, kunde na chumvi wanufaika watapewa fedha taslimu.
Utoaji wa fedha taslimu unawapa wakimbizi uhuru wa kuchagua chakula gani cha kununua na wakati huohuo kuingiza fedha katika uchumi wa ndani. Soko la Pamoja la Nyarugusu, lililofunguliwa mwaka huu, ni eneo huru kati ya kambi na jamii ya wenyeji, ambako wafanyabiashara wanapata nafasi ya kuwauzia wakimbizi bidhaa zao.
“Canada inafurahi kusaidia shughuli za WFP za kuhudumia wakimbizi nchini Tanzania,” alisema Mheshimiwa Ian Myles, Balozi wa Canada nchini Tanzania. “Kuunganisha msaada wa chakula na fedha taslimu kunawapa wanawake na wanaume uhuru zaidi katika kukidhi mahitaji yao na kunaweza kuwa na matokeo mazuri kwa jamii ya wenyeji.”
Zaidi ya wakimbizi robo milioni wamepata hifadhi nchini Tanzania katika kambi tatu magharibi mwa nchi. Wakimbizi nchini Tanzania, hususan kutoka katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wanategemea sana msaada wa WFP kama chanzo chao kikuu cha chakula.
Kabla ya kuanza kwa mradi wa majaribio wa fedha taslimu, wakimbizi walikuwa wakipokea msaada wa chakula tu kutoka WFP. Kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Tanzania, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na washirika wengine, mradi wa majaribio wa fedha taslimu unasaidia baadhi ya kaya zilizo hatarini zaidi za wakimbizi katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu.
“Kutoa fedha taslimu kwa wakimbizi kunawajengea uwezo wa kufanya uaumzi wao kuhusu chakula kipi wanunue na kupika nyumbani,” alisema Michael Dunford, Mwakilishi wa Nchi wa WFP Tanzania. “Fedha taslimu huwapa wakimbizi fursa ya kula vyakula tofautitofauti, na hivyo kuwasaidia kubadili mlo wao.”
WFP inalenga kuongeza idadi ya wakimbizi wanaopokea fedha taslimu badala ya masaada wa chakula katika mwaka wa 2017.
Tangu kuanza kwa machafuko ya kisiasa nchini Burundi mwezi Aprili, 2015, takribani Warundi 190,000 wametafuta hifadhi nchini Tanzania. Kwa kuunganisha na idadi ya wakimbizi waliokuwepo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Tanzania hivi sasa inahifadhi zaidi ya wakimbizi robo milioni. Mamia ya wakimbizi wanaendalea kuwasili kila siku kutoka Burundi.
WFP inahitaji takribani Dola za Marekani milioni 6 kwa mwezi ili kuendelea kuwasaidia wakimbizi katika mwaka 2017 ambao idadi yao inaendelea kuongezeka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...