Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Ugunduzi wa gesi asilia nchini umepelekea kushuka kwa gharama za umeme kwa asilimia 33.26 kwa mwaka 2014 hadi 2016.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani ameyasema hayo leo Bungeni, Mjiji Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge viti Maalum Maida Hamad Abdallah kuhusu faida zilizopatikana tangu kugundulika kwa gesi asilia.
“Faida kubwa iliyopatikana kutokana na ugunduzi na matumizi ya gesi asilia nchini ni uzalishaji wa umeme wa bei nafuu kwa kutumia Gesi Asilia ikilinganishwa na mafuta. Uzalishaji umeme kwa kutumia Gesi Asilia umeongezeka kutoka uniti 2,714.25 milioni kwa mwaka 2014 hadi uniti 4,196.4 milioni mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 54.61,” alifafanua Dkt. Kalemani.
Aliendelea kwa kusema kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa Gesi Asilia umepelekea kushuka kwa bei ya umeme kutoka wastani wa shilingi 188.56 kwa uniti mwaka 2014 hadi wastani wa shilingi 125.85 kwa uniti mwaka 2016.
Akitolea ufafanuzi zaidi juu ya faida zinazopatikana kutokana na matumizi ya Gesi Asilia, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa maeneo ya Mikocheni, Jijini Dar es Salaam zikiwemo nyumba za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wanatumia Gesi Asilia ambapo gharama wanayoitumia kwa mwezi haizidi shilingi elfu 25,000, na wanatumia kwa kupikia aina zote za vyakula hata vile vinavyotumia muda mrefu kuiva kama vile maharage na makongoro.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...