Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Nile “Nile Day” yatakayofanyika wiki
ijayo (Februari, 22), jijini Dar es
Salaam.
Maadhimisho hayo
yameandaliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na taasisi
inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile-Nile Basin Initiative (NBI).
Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Mha. Gerson Lwenge ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akiongea
na mwandishi wa habari hii kuhusu maadhimisho hayo.
Mha. Lwenge amesema
kuwa maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka miongoni mwa nchi wanachama 10 zilizo
katika bonde la mto huo; ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi,
Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Sudan ya Kusini na Misri,
ambapo kwa mwaka huu siku hiyo inasherekewa nchini Tanzania.
“Lengo la Siku ya Nile ni kukuza uelewa kwa watu
wote kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zote wanachama, masuala yanayotekelezwa
na faida inayopatikana kutokana na matumizi bora ya rasilimali za Bonde la Mto Nile,”
alisema Mha. Lwenge.
Amefafanua
kuwa maadhimisho hayo yatasaidia kufahamu zaidi kuhusu umuhimu wa mto huo
katika kutupatia chakula cha uhakika, maji, nishati ya umeme na faida nyingi
kiuchumi pamoja na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kulinda na kutumia rasilimali
za mto huo kwa pamoja na kwa usawa na uendelevu kwa ajili ya kizazi cha leo na vizazi
vijavyo.
Mha.
Lwenge ameongeza kuwa maadhimisho hayo yataambatana na maandamano kutoka
viwanja vya Mnazi Mmoja mpaka Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere, upandaji wa miti, maonesho ya vitu mbalimbali vinavyohusu Sekta za
Maji na Umwagiliaji, burudani za kiutamaduni, pamoja na za watoto wa shule za
msingi na sekondari.
Aidha,
Waziri Lwenge amewataja washiriki wa maadhimisho hayo kuwa ni mawaziri
wanaohusika na maji kutoka nchi wanachama, mabalozi, wawakilishi kutoka NBI, wabunge,
washirika wa maendeleo, wataalamu, wanafunzi wa vyuo, sekondari na shule za msingi,
taasisi binafsi, vyombo vya habari pamoja na umma kwa ujumla.
NBI
ilianzishwa rasmi mwaka 1999, jijini Dar es Salaam, ambapo nchi wanachama
waliungana na kukubaliana kuanzisha umoja wa ushirikiano katika kusimamia na
kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...