Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi jana aliwatambelea Watanzania wanane
wanaoshikiliwa katika Gereza Kuu la Mzuzu nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia
kinyume cha sheria katika mgodi wa urani wa Kayerekera.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu alifuatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa
Ruvuma, Bw. Hassan Bendeyeko pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo
ya Nje na Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi,aliwasihi watu hao kuwa wavumilivu
wakati Serikali ikitafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Balozi Mwinyi aliwaeleza Watanzania hao kuwa mazungumzo katika
ngazi mbalimbali kati ya Tanzania na Malawi yanaendelea na kuna matumaini
makubwa kuwa hivi karibuni ufumbuzi wa suala lao unaweza kupatikana.
Balozi Mwinyi aliendekea kuekeza kuwa yeye na wenzake wamekuja
Lilongwe kushiriki kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC)
kati ya Tanzania na Malawi, lakini
wameamua kusafari takriban kilomita 400
kutoka Lilongwe hadi Mzuzu kuja kuwaona
na kuwafikishia ujumbe kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha kuwa suala
hili linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
"Nikufahamisheni kuwa jitihada katika ngazi mbalimbali kwa
ajili ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo lenu zinaendelea na hata Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokutana na
Rais wa Malawi, Mhe. Prof. Peter Mutharika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa
Nchi wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia jambo lenu lilikuwa moja ya
masuala waliyoyajadili.
Naibu Katibu Mkuu alisema kuwa alifarijika kuwakuta watu hao wote
wapo salama na wenye afya nzuri na kuwajulisha kuwa ziara hiyo ya kuwatembelea
na nyingine zilizofanyika siku za nyuma ni ushahidi dhahiri kwao na kwa
Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. Magufuli imedhamiria kuwahudumia Watanzania
wote wa kada mbalimbali popote pale wanapoishi.
Watanzania hao wanane walikamatwa mwishoni mwa mwezi Desemba, 2016
na hadi sasa wanashikiliwa katika gereza kuu la Mzuzu. Watanzania hao ambao
kati yao wawili ni wanawake
wamejitambulisha ni wakulima na wachimbaji wadogo wa madini wanatoka
katika mkoa wa Ruvuma na walikwenda Malawi chini ya Taasisi ya CARiTAS
kujifunza athari za migodi ya urani katika jamii.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...