Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo vya kazi Mabalozi wapya watatu
ambao aliweteua tarehe 3 Disemba 2016.
Mabalozi hao ni Mhe. Joseph Sokoine
anayekuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Omar Yussuf Mzee anayekuwa
Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Algeria na Mhe. Grace Mgavano anayekwenda
kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Dkt. Ladis Komba nchini Uganda ambaye
alistaafu kwa mujibu wa sheria.
Balozi Sokoine ambaye anakwenda kujaza nafasi
iliyoachwa wazi na Mhe. Deodorus Kamala ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara
ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Balozi Mzee kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo
alishawahi kushika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nafasi ya mwisho alikuwa Waziri
wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika awamu ya kwanza ya Mhe. Rais Dkt. Ali Mohammed Shein.
Kwa upande wa Balozi Mgavano kabla ya kuteuliwa
kushika wadhifa wa Ubalozi alikuwa Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Rais, Ikulu.
Mabalozi wote waliopangiwa vituo vipya vya kazi
wataapishwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kesho siku ya Jumapili tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu
jijini Dar Es Salaam saa tano asubuhi.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki,
Tarehe 11 Februari 2017
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...