Taasisi isiyo ya kiserikali ya Land O’ Lakes imewaomba wadau wa kilimo
na biashara nchini kushiriki kwenye harambee inayolenga kukusanya fedha kiasi
cha Tsh 150 milioni kwa ajili ya kuwezesha mradi wa kuwajengea uwezo wanawake
waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara, inayotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi.
Harambee hiyo inayotarajiwa
kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa itafanyika jijini Dar es Salaam, huku
kiasi cha fedha kitakachopatikana kikitarajiwa kuelekezwa katika kuijengea
uwezo wa kiutendaji taasisi inayojihusisha na kuendeleza wanawake
katika kilimo Tanzania (CAWAT).
Harambee hiyo imebeba kauli mbiu: ‘Wezesha kilimo biashara kwa ajili ya ajira,
jamii na viwanda endelevu’.
“Mafanikio tutakayoyapata
kupitia harambee hii yataiwezesha CAWAT kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo
wanawake wanaojishughulisha na kilimo hapa nchini kubadilika na kujikita zaidi
katika kilimo biashara kwa maana kwamba watajengewa uwezo wa kufahamau fursa za
masoko ya bidhaa wanazozalisha, kujitangaza pamoja kuwaunganisha na wawekazi
wakubwa,’’ alisema Mkurugenzi wa Mradi kutoka
Land O’ Lakes, Dk Rose
Kingamkono.
Hatua hiyo inakuja huku
takwimu zikionyesha kwamba zaidi ya asilimia 70 ya watu hapa nchini wanaishi
vijijini na kwamba asilimia 98 ya wanawake wanaoishi vijijini wanajishughulisha
zaidi na kilimo ambacho hata hivyo kinachangia asilimia 26 ya pato la nchi.
“Pamoja
na wanawake kuwa wahusika wakuu na wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za
awali za kilimo, mara nyingi wamekuwa hawafaidiki na jasho la kazi zao.Hali hii
ni kwa kuwa wanaume wamekuwa wakihodhi masuala yote yanayohusiana na faida
zitokanazo na kilimo kwa kuhusika zaidi mwisho wa mnyororo wa kilimo ikiwemo
masoko,’’
“Ni katika mazingira kama hayo ndipo unaonekana
umuhimu wa kuwekeza jitihada zetu za hali na mali katika kuhakikisha kwamba
huyu mwanamke ambae hanufaiki na jasho lake licha kusota katika msimu wote wa
kilimo sasa ananufaika na hili litawezekana iwapo atajengewa uwezo wa kufanya
kile ambacho jamii inaamini mwanamke hawezi kukifanya yaani kilimo biashara,’’
aliongeza Dk Kingamkono katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Akizungumzia kuhusu taasisi ya CAWAT, Mwenyekiti wa
Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi hiyo
Dk
Victoria Kisyombe, alisema kwa sasa ipo kwenye mchakato wa awali wa kuanza kujitegemea yenyewe
kiuendashaji bila kutegemea msaada iliyokuwa ikiupata kutoka kwenye mradi
unaohusu Ubunifu katika masuala ya kijinsia na kuimarisha uhakikaka wa chakula
katika ngazi ya kaya (IGE), unaotarajiwa kuisha Machi
mwaka huu.
“Kuelekea katika
kujiendesha yenyewe bila kutegemea msaada tunaoupata kutoka mradi wa IGE, CAWAT
tunaona kwamba tuna safari ndefu inayohitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali
wa maendeleo ili tuweze kutimiza wajibu wetu wa kuwasaidia wakina mama walio
kwenye sekta hii muhimu ya uzalishaji. Tunawaomba sana watanzania mmoja
mmoja, taasisi, mashirika, balozi mbalimbali waguswe katika kusaidia hili.’’ Alisema Dk. Kisyombe.
Mkurugenzi wa Mradi wa Ubunifu Katika Maswala ya Kijinsia na Kuimarisha Uhakika wa Chakula Katika Ngazi ya Kaya, unaoendeshwa na taaisisi ya Land O Lakes, na kufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Watu wa Merekani (USAID), Dk Rose Kingamkono (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na harambee iliyoitishwa na taasisi hiyo kesho Alhamisi ikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake katika kilimo biashara kupitia taasisi iliyojikita kwenye kuendeleza wanawake katika kilimo Tanzania (CAWAT). Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya CAWAT Dk. Victoria Kisyombe.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya CAWAT Dk. Victoria Kisyombe (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na harambee itakayofanyika kesho (Alhamisi) jijini Dar es Salaam ikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake katika kilimo biashara. Kulia ni Mkurugenzi wa Mradi wa Ubunifu Katika Maswala ya Kijinsia na Kuimarisha Uhakika wa Chakula Katika Ngazi ya Kaya, unaoendeshwa na taaisisi ya Land O Lakes, Dk Rose Kingamkono (kushoto)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...