Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa (Mb) kesho (28 Februari 2017) atafungua mkutano wa siku moja wa
Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Bodi za Mashirika ya Umma utakaojadili nafasi
za Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa II wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano.
Mkutano huu ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina utafanyika Ikulu – Dar es Salaam kuanzia
saa 2.30 asubuhi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi
ya Uongozi Profesa Joseph Semboja
amesema kwamba malengo ya mkutano
ni kukusanya maoni ya viongozi kuhusu nafasi ya Mashirika ya Umma katika
utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; kuzungumzia
changamoto tarajiwa katika utekelezaji wa majukumu haya na; kutoa mapendekezo
ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
“Mashirika ya Umma yana nafasi na uwezo mkubwa wa
kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano,
2016/17–2020/21 wenye kaulimbiu ‘Maendeleo
ya Viwanda kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu’,” alisema
Profesa Semboja.
Profesa Semboja aliendelea, “Katika kuunga mkono
jitihada za Serikali ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli mkutano huu unawakutanisha
viongozi kutoka Serikalini na Mashirika ya Umma kwa lengo la kubadilishana
maarifa na uzoefu wa jinsi mashirika haya yatakavyoiwezesha Tanzania kuwa nchi
ya viwanda kwa maendeleo endelevu.”
Pamoja na mambo mengine, mkutano utajadili namna
ya kuboresha mifumo
ya kiundetaji ndani ya mashirika na
mahusiano miongoni mwa mashirika na taasisi za Serikali; kufungamanisha
mipango ya mashirika ya Umma na Mpango wa Pili wa Maendeleo; kutathmini kiwango na aina ya rasilimali zinazohitajika kuwezesha utekelezaji wa mipango na; kufanya
ufuatiliaji na tathmini
ya mipango.
Mkutano utawakutanisha zaidi ya washiriki 100
kutoka Wizara, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Udhibiti takribani 52 hapa
nchini.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano –Taasisi ya Uongozi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...