Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wa hapa nchini wametakiwa kuyahimiza makampuni ya nchi yao kutumia fursa za uwekezaji zinazotokana na zoezi la Serikali la kuhamia Dodoma. 

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) katika kikao maalum cha kuwafahamisha wanadiplomasia hao uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuhamia Dodoma.

“Uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mjini Dodoma umetengeneza fursa nyingi za uwekezaji katika maeneo mbalimbali kama vile utengenezaji wa vifaa vya ujenzi; ujenzi wa majengo ya ofisi, biashara na makazi; huduma za kijamii kama hospitali, shule, miundombinu ya maji safi na maji taka; TEHAMA; bustani za mapunziko; shughuli za kilimo na utalii. Hivyo, nachukua fursa hii kuwaomba muwahimize wawekezaji kutoka nchi zenu kuchangamkia fursa hizo”, Balozi Mahiga aliwambia wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza katika Mkutano na Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wa hapa nchini, kuhusu zoezi la Serikali la kuhamia Dodoma. mazungumzo hayo yalifanyika leo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam. Kushoto kwa Mhe. Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima.

Balozi Mahiga alieleza kuwa uamuzi wa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar Es Salaam kwenda Dodoma ulifanywa mwaka 1973 lakini tokea kipindi hicho haukuweza kutekelezwa kutokana na sababu mbalimbali hadi Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilipoingia madarakani.

Mhe. Waziri alieleza kuwa zoezi la Serikali kuhamia Dodoma limepangwa kutekelezwa kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza tayari imeshakamilika. Katika awamu hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imehamisha watumishi 47 kati ya 152 waliopo Makao Makuu akiwemo yeye mwenyewe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. 
Waziri Mahiga aliendelea kueleza kuwa kufuataia kuanza utekelezwaji wa uamuzi huo ambao ulitangazwa rasmi na Mhe. Magufuli alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM tarehe 23 Juali 2016, hakuna budi kwa Ofisi za Balozi na Mashirika ya Kimataifa nazo zianze kujiandaa kwa ajili ya kuhamia mji huo Mkuu wa Serikali.  

Aliongeza kuwa, katika kipindi hiki cha mpito, baadhi ya Watumishi wa Wizara watakuwepo Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine watasaidia mawasiliano na ofisi hizo. Aidha, katika kipindi hicho, Wizara katika ofisi zake mpya zilizopo kwenye Jengo la LAPF mjini Dodoma itaimarisha mawasiliano kwa njia ya simu, mtandao wa internet na kufunga kifaa cha kufanyia mikutano kwa njia ya video ili kurahisisha mawasiliano na ofisi za Balozi.

Mhe. Mahiga aliwafahamisha Mabalozi hao kuwa Serikali itatenga eneo maalum ambalo litakuwepo kwenye mji wa Serikali utakaojengwa Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za balozi na mashirika ya kimataifa.  Alisema pindi Serikali itakapokamilisha zoezi la kupitia upya Mpango Mkuu wa Mji wa Dodoma, itawasiliana na Balozi hizo ili ziweze kuwasilisha maombi ya mahitaji ya ardhi wanayohitaji.
Balozi Mahiga alihitimisha kikao hicho kwa kuwashauri wanadiplomasia wanaomiliki majengo jijini Dar es Salaam kuingia makubaliano maalum na kampuni zinazohitaji ofisi hapa jijini ili kampuni hizo ziwajengee majengo ya ofisi mjini Dodoma. 

Kwa ujumla wanadiplomasia walipokea uamuzi huo na kuiomba Wizara iwasilishe taarifa hiyo kwa maandishi ili nao waiwasilishe kwenye Serikali zao kwa ajili ya utekelezaji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...