Serikali imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya kukagua barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.
“Najua bado kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria”, amesema Profesa Mbarawa.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzingatia viwango na kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo hicho ili kiweze kufikia hatua ya kujenga barabara nchini.
Aidha, amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda na kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiruka mtaro wa maji uliopo pembezoni mwa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera. Barabara hiyo inajengwa na mkadarasi kutoka Kampuni ya CHICO na imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 64.96.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mhandisi Jumanne Werema (wa kwanza kulia), kuhusu kukamilisha ujenzi kwa wakati wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
Mhandisi Jumanne Werema kutoka Kampuni ya ujenzi wa CMG akimpa taarifa ya mradi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wakati alipokagua, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...