Watanzania wametakiwa kumuunga mkono Rais John Magufuli kwenye vita ya kulinda rasilimali za nchi aliyoianzisha kwani kwa muda mrefu watu wachache walishiriki kufuja mali za nchi ambazo zingetumika kwa manufaa ya watu wengi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Starnley Kamoga aliyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya albino duniani, ambayo kimkoa ilifanyika kituo cha 4 Angle mji mdogo wa Haydom, alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huo Dr Joel Nkaya Bendera.

Alisema vita ya kulinda rasilimali ya nchi inapaswa kuungwa mkono kwani utajiri wa nchi ya Tanzania haulingani na hali halisi iliyopo kutokana na watu wachache kupora utajiri kupitia madini mbalimbali.

Alisema ana imani Rais Magufuli na watanzania kwa ujumla watashinda vita ya kulinda rasilimali kwani kupitia ripoti ya pili ya makania imeonyesha namna wananchi wanyonge wanavyoibiwa.

“Pamoja na kuathimisha siku ya albino duniani tunapaswa kumuunga mkono Rais Magufuli katika vita hii ya kusimamia na kulinda rasilimali za nchi kupitia madini yetu kwani nia ya dhati ameionyesha,” alisema Kamoga.

Alisema aliwaagiza watumishi wa halmashauri hiyo waangalie kwenye runinga na yeye mwenyewe aliiangalia ripoti hiyo kwa lengo la kumuunga mkono Rais Magufuli katika kusimamia rasilimali zilizopo kwenye eneo hilo.

"Ukiisikiliza kwa makini hiyo taarifa ya pili ya makinikia na sisi ambao tunafanya kazi ya kumsaidia Rais kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha kuwa wananchi wanyonge wanafaidika na rasilimali waliyonayo unaweza ukalia kwa sababu hali iliyopo ni tofauti na uhalisia," alisema Kamoga.

Alisema wananchi na viongozi wanapaswa kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli na endapo dhamira ya dhati itakuwepo kwa wote rasilimali za nchi zitawanufaisha wananchi wote.

Naye, Mwenyekiti wa chama cha maalbino mkoani Manyara, Joseph Masasi alisema wanakabiliwa na changamoto ya kutobaini idadi kamili ya watu wenye ualbino mkoani humo hivyo kukosa takwimu sahihi.

Masasi alisema tatizo hilo linasababisha hata kukitokea tatizo lolote linalohitaji msaada kwao inakuwa vigumu kwani wengine wanakosa kutokana na kutobainishwa kwa idadi yao katika wilaya za mkoa huo.

Alisema pia wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mafuta maalum ya kujipaka kwa watu wenye ualbino yanayowasaidia kila siku ili wasiathiriwe na mionzi ya jua na kusababisha baadhi yao kuathirika.

“Pamoja na hayo tunashukuru kwenye mkoa wa Manyara hakuna matukio ya watu wenye ualbino kuuawa au kukatwa viungo na watu makatili ila kuna badhi ya matishio madogo madogo,” alisema Masasi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Joseph Mandoo alisema halmashauri yao itaendelea kushirikiana na uongozi wa ualbino kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa msaada unaohitajika kwa watu hao.

Mandoo alitoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ualbino kutowafisha ndani na badala yake wawafikishe kwenye sehemu husika ili pindi misaada itakapotolewa waweze kupatiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Starnley Kamoga, akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) katika maadhimisho ya siku ya albino duniani ambayo kimkoa ilifanyika Mji mdogo wa Haydom wilayani Mbulu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...