Na Mwandishi wetu, Bagamoyo: Makampuni ya Kimataifa na Kitaifa yanayoendesha shughuli za kibiashara hapa nchi makubwa kwa
madogo yanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa kuheshimu haki za binadamu na kuwajibika pale
yanapokiuka haki hizo.
Hayo yameelezwa leo mjini Bagamoayo na Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Obadia
Kameya, wakati akifungua mafunzo ya uwezeshaji kwa Maafisa wa Serikali kuhusu Biashara na Haki za
Binadamu. Bw. Kameya amesema, Makampuni ambayo yatabainika kukiuka haki za binadamu katika uendeshaji
wa shughuli zao, yanapashwa kuchukuliwa hatua na kwamba mwenye wajibu huo ni Serikali ambayo
ndiyo inayobeba dhamana kwa mujibu wa Katiba ya kuhakikisha kwamba haki za wananchi wake ndani
ya mipaka yake zinalindwa, kusimamiwa na kutetewa.
Ni kwa sababu hiyo, Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema, Maafisa wa Serikali
ambao kwa namna moja ama nyingine wanahusika na masuala ya Biashara na Haki za Binadamu
wanapashwa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu Kanuni na Miongozo inayohusu Haki za Binadamu na
Biashara.
Akasema , suala la Biashara na Haki za Binadamu limekuwa ajenda ya ulimwengu katika miaka ya hivi
karibuni kutokana na kuhusishwa kwake na haki za binadamu na ni katika muktadha huo Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama Mshauri wa Serikali kuhusu mauala ya Sheria, imeamua kwa
Kushirikiana na Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Kanda ya Afrika (OHCHR-EARO)
kuandaa mafunzo ya kuwajenga uwezo Maafisa wa Serikali.
Bw. Kameya akasisitiza zaidi kwa kueleza kwamba, ni muhimu sana kwa Maafisa katika Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Maafisa kutoka Wizara nyingine za Serikali na Taasisi kuwa
na utambuzi wa masuala ya Biashara na Haki za Binadamu ambayo yaathari kwenye sera, sheria,
mikataba na makubaliano ya kimataifa na katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali na
hasa katika kipindi hiki ambacho nchi imejielekeza kuwa nchi ya Viwanda.
Naye Mwakilishi wa OHCHR EARO Madame Nwanneakolam Vwede-Obahor amesisitiza kwamba ingawa
Maaofisa wa Serikali wanaowajibu wa msingi kabisa wakuhakikisha kwamba wanafuatilia kwa karibu na
kuhakikisha kwamba Makapuni ya Kibashara yatekeleza na kuwajibika katika kuhakikisha kwamba
hayakiuki misingi na kanuni za haki za binadamu na kwamba yajifanyia tathimini na kutoa taarifa kama
inavyotakiwa.
Wawezeshwaji wa Mafunzo hayo wakiongozwa na Madame Nwanneakolam Vwede-Obahor ambaye ni
Mwakilishi wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Kanda ya Afrika ( OHCHR-EARO)
walifundisha kuhusu Mfumo wa Umoja wa Mataifa ulioridhiwa mwaka 2008 unaojulikana kama Zuia,
Heshimu na Fidia kuhusu Biashara na Haki za Binadamu.
Mfumo huu wa Umoja wa Mataifa una Misingi Mikuu Mitatu. Wa Kwanza ni kuhusu wajibu wa serikali
kwa kuzingatia sheria ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ya kumlida kila mtu ndani ya mipaka yake na
katika eneo la mamlaka yake kwa kuweka sheria madhubuti , kanuni , sera ikiwa ni pamoja na kuzuia
na kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Makampuni ya Kibiashara.
Msingi wa Pili wa mfumo huu unazitaka Kampuni za Biashara kuwajibika katika kuheshimu haki za
binadamu mahali popote zinakoendesha shughuli zao bila ya kujali ukubwa au udogo wa biashara hiyo
ikiwa ni pamoja na kutambua madhara yatokanayo na shughuli zao na kuchukua hatua za kuzuia
madhara hayo.
Msingi wa Tatu ni utoaji wa fidia kutokana na athari za ukiukwaji wa haki za binadamu unaotokana na
shughuli za kibiashara zinazofanywa makampuni hayo. Baadhi ya athari hizo zinatajwa kuwa ni pamoja
na uchafuzi wa mazingira, ajali kazini, malipo au ujira duni, uhamishwaji wa kutumia nguvu na
usiozingatia sheria.
Washiriki wa Mafunzo hayo wametoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Mambo ya
Ndani, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Biashara na Viwanda, Tume ya
Kurekebisha Sheria , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Kituo cha Uwekezaji, Nishani na Madini, na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Washiriki wa Mafunzo ya Uwezeshaji kuhusu Biashara na Haki za Binadamu wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo. mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika mjini Bagamoyo na yameandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kanda ya Afrika (OHCHR EARO). Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Obadia Kameya aliyeketi katikati kushoto kwake ni Madame Nwanneakolam Vwede-Obahor na kulia ni Bi. Cecilia S. Shelly- Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Pwani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...