Na Georgina Misama – MAELEZO
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
imewaonya watumishi wa Umma kutoa taarifa za serikali za siri na za kawaida kwa
watu ambao sio walengwa wa taarifa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa
Maadili kutoka Wizara hiyo Lambert Chialo alisema kwamba kwa mujibu wa sheria ya
Usalama wa Taifa Na. 3 ya mwaka 1970 na marekebisho yake, Ibara ya 5(a) na (b),
adhabu ya uvujaji wa siri ni kifungo kisichozidi miaka 20.
“Hivi karibuni tumeshuhudia taarifa za serikali za siri zikitumwa katika vyombo vya
habari pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii kitu ambacho ni kosa kisheria na ni
kinyume cha Kanuni za Maadili ambapo inasisitizwa kuwa na matumizi sahihi ya
taarifa”, alisema Chialo.
Chialo aliongeza kwamba lengo la serikali si kuficha taarifa kwa wadau wake, bali
taarifa zinazotolewa zinapaswa kutolewa kwa utaratibu maalumu na kupelekwa kwa
watu wanaopaswa kupokea taarifa hizo (walengwa). Aidha, taarifa zinazotolewa na
taasisi husika lazima zipate idhini kwa Uongozi husika kabla ya kupelekwa kwa wadau.
Akiongelea suala la matumizi mabaya ya Ofisi, Chialo alisema kwamba baadhi ya
watumishi wamekuwa wakitumia nafasi walizonazo kwa manufaa yao binafsi na sio ya
Umma, kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na watumishi watakaogundulika
watawajibishwa kwa mujibu wa Kanuni na taratibu.
Watumishi wa Umma wanapaswa kufahamu kwamba serikali inaendelea kufatilia
matendo yote yasiyo ya kimaadili na kuchukua hatua kila inapobidi. Aidha, wananchi
wanaombwa kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili katika taasisi
za umma kila wanaposhuhudia matukio hayo.
“Tunalo dawati la msaada kwa ajili ya kupokea maoni, malalamiko, ushauri na taarifa
mbalimbali katika kuhakikisha utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi
unaboreshwa” alisema Chialo.
Chialo alitoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla, kuzingatia swala la maadili kuanzia
ngazi ya familia. Aidha, inasisitizwa viongozi na wasimamizi wa kazi kuendelea
kuelimisha watumishi kuhusu suala la maadili na kuhakikisha watumishi wanaishi kwa
kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa vitendo.
Kaimu Mkurugenzi wa Maadili toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Bw. Lambert Chialo (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) wakati akieleza umuhimu wa watumishi wa Umma kuzingatia maadili kazini, kulia ni Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Bi. Mary Mwakapenda.
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...