Jonas Kamaleki- MAELEZO

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezitaka nchi wanachama wa Kituo cha Madini na Kijiosayansi cha Afrika (AMGC) kuweka mazingira rafiki kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, kuandaa raslimali watu na vitenda kazi ili kuifanya sekta kutoa tija.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa 37 wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Madini na Kijiosayansi cha Afrika.
Majaliwa amesema kuwa raslimali madini inaweza kuwa chanzo cha kusukuma maendelo ya uchumi katika nchi nyingi Barani Afrika kama ikisimamiwa vema.

“Changamoto kuu kwa sasa ni jinsi gani tunaweza kuwa na sekta ya madini inayotoa mchango stahiki katika nchi husika na Bara la Afrika kwa ujumla,” amesema Majaliwa.Aliongeza kuwa taarifa za kijiolojia zinaonyesha kuwa Afrika ni Bara lenye utajiri mkubwa wa raslimali madini na mengi kati yao bado hayajaanza au yako kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.

Aidha, Waziri Mkuu amesema lengo la uanzishwaji wa kituo hiki ni kuhakikisha sekta ya madini inawajibika kuleta maendeleo ya kijamii na uchumi pia ikijali masuala ya mazingira.Amezitaja kazi za AMGC kuwa ni kutafi,kufundisha wataalaam pia kusimamia maabara ya kisasa kwa ajili ya uhakiki na uongezaji thamani wa madini, hivyo amehimiza watanzania na nchi nyingine wanachama kukitumia kituo hicho.

Waziri Mkuu amesema kuwa kituo hiki kikitumika vema kinaweza kutoa tija kubwa kwenye sekta ya uchimbaji wa madini,uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta ambapo pia masuala ya usimamizi wa mazingira utazingatiwa.

“Tanzania licha ya kuwa na utajiri wa madini ya Dhahabu, Almasi,Shaba,Chuma, Madini ya vito kama Tanzanite na mengineyo, mchango wa sekta ya madini ni asilimia 4.8 ya pato ghafi la Taifa,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa kuna haja ya kuongeza usimamizi wa sekta hiyo ili kutoa tija kusudiwa kwa nchi ya Tanzania.

Waziri Mkuu pia amezitaka nchi wanachama kulipa ada zao kwa AMGC kwa wakati ili kuondoa changamoto ya raslimali fedha katika kituo hicho.Ameyasema hayo baada ya kupata taarifa kuwa zipo nchi nyingi ambazo hazilipi ada zao kwa wakati na nyingine kulimbikiza madeni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa AMGC ni kituo muhimu kwa maendeleo ya Tanzania hususan katika sekta ya Madini.Ameongeza kuwa kituo hicho kitakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania kwani kitaweka mitambo ya kuchenjua madini jambo ambalo linaunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuli za kuzuia makinikia kusafirishwa nje.

Mtambo huo utaongeza ajira nchini kwa kuwa kituo hicho kipo Tanzania. Na amezisihi nchi nyingine za kiafrika kujiunga na AMGC na kuongeza kuwa nchi 36 za Afrika zimeonyesha nia ya kujiuinga.Mkutano huu umeenda sanjari na maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa AMGC mwaka 1977 ambapo Mhe Waziri Mkuu amekata keki kuashiria sherehe hizo.

Tanzania ndio Mwenyekiti wa Mkutano huu na wajumbe wameonyesha nia ya kuiomba Tanzania iwe Mwenyekiti kwa mwaka mwingine kutokana na msimamo imara wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kusimamia raslimali za madini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika picha ya pamoja na Wanachama wa nchi za Kituo cha Madini na Kijiosayansi cha Afrika (AMGC) leo tarehe 14/09/2017 baada ya kufungua Mkutano wa 37 wa Baraza la Uongozi wa kituo hicho.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata keki ikiwa ni ishara ya Maadhimisho ya miaka 40 ya Kituo cha AMGC tangu kuanzishwa kwake. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu kituo cha AMGC, Ibrahim Shaddad , kushoto ni Mwenyekiti wa AUC, Frank Mugenyi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea kwenye maabara mbalimbali katika kituo cha AMGC. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu kituo cha AMGC, Ibrahim Shaddad na kulia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani. Wengine ni washiriki wa mkutano huo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kituo cha AMGC.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mtaalam Mshauri wa kituo cha AMGC, Timo Gawronski kuhusu namna Maabara ya Kisasa ya Upimaji Madini ambayo inaonesha asili ya madini ya mahali yaliyochimbwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...